WAZIRI MWAKYEMBE AZITAKA OFISI ZA UMMA KUTOA TAARIFA KWA WANAHABARI

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma


Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imezitaka ofisi za Umma kutoa taarifa kwa wanahabari kwa kuwa siyo hisani na siyo hiyari, bali ni takwa la kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 (d).


Kauli hiyo imetolewa na Waziri mwenye dhamana ya tasnia ya Habari Dkt. Harrison Mwakyembe alipokutana na ujumbe wa viongzi wa Chama cha Waandishi wa Habari kutoka mkoani Arusha pamoja na Asasi ya Vyombo vya Habari Mbadala (Alternative Media) leo jijini Dodoma.


“Serikali haina ugomvi na vyombo vya habari, bila vyombo vya habari hatutaweza kuwahabarisha wananachi masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu” amesema Dkt. Mwakyembe.


Aidha, amewakumbusha wanahabari kuwa kazi wanayofanya ni muhimu sana ambapo nchi zilizoendelea bado wanatumia vyombo vyao vya habari ikiwemo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ambalo lina miaka zaidi ya 90 na linatangaza habari zake kwa lugha zaidi ya 40 ili kuwafikia wananchi wake na dunia kwa ujumla.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari kutoka mkoa wa  Arusha Bw. Claud Gwandu amemshukuru Waziri Dkt. Mwakyembe kwa mapokezi, majadiliano yenye tija kwa uwazi na ukweli na kumpongeza kwa kazi nzuri anayofanya katika sekta anazozisimamia.


“Tunamshukuru Waziri kwa kutupa nafasi ili tuweze kushirikiana katika kuimarisha tasnia ya habari iwe bora kwa mustakabali wanchi yetu” amesema Gwandu.


Aidha, Mwenyekiti huyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya kwa kutekeleza miradi mingi kwa manufaa ya Watanzania na kusisitiza kwa mwenye macho haambiwi tazama.


…MWISHO..


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527