WAKAMATWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA KUMUUA BABA YAO MZAZI


Jeshi la Polisi mkoani Katavi linawashikilia watu wanne,watatu wakiwa familia moja kwa tuhuma za kumuua kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni na sehemu za siri Baba yao Lumba Nhalima(57).

Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 3 usiku katika kijiji cha Kasekese wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi wakati marehemu akitoka kunywa pombe na kuelekea nyumbani.

Akithibitisha tukio hilo,Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi Benjamin Kuzaga alisema, siku ya tukio watuhumiwa walimnywesha pombe nyingi marehemu ili ashindwe kujitambua kwa lengo la kumdhuru.

Kwa mujibu wa kamanda Kuzaga ni kwamba,marehemu akiwa njiani kurudi nyumbani alikutana na watuhumiwa hao ambao ni Sali Lumba(32) Jonas Lumba(28) na Paulo Lumba(19) na mtu mwingine ambaye alikuwa anakunywa naye pombe marehemu aliyetambulika kwa  Thomas Malongo(54)

Kuzaga alisema, baada ya uchunguzi jeshi la Polisi limebaini kuwa, kabla ya kifo  chake marehemu alikuwa akilalamika kuwa watoto wake wanne ambao ni wa mke mkubwa aitwaye Wande Mabuki(46) wanataka kumuuwa ili  yeye na watoto warithi mali zake.

Hata hivyo Kuzaga alisema, chanzo cha kifo hicho kinahusishwa na Imani za kishirikina pamoja na tamaa za kurithi mali, kwa hiyo Jeshi la Polisi linaendelea kufanya msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wengine waliohusika katika tukio hilo.

Aidha Kamanda Kuzaga amesema, baada ya mahojiano ya kina watuhumiwa hao wanne wamekiri kuhusika kupanda njama na kufanikisha mauaji.

“Jeshi la polisi linatoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Katavi kuachana na dhana potofu za kujipatia kipato kwa njia ambazo si halali ikiwemo njia za kishirikina” alisema Kamanda Kuzaga.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post