MBUNGE WA KISHAPU SULEIMAN NCHAMBI KUENDELEA KUSOTA RUMANDE..KESI YAKE YA UHUJUMU UCHUMI YAPIGWA KALENDA HADI MEI 25


Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga Suleiman Masoud Nchambi (CCM), imetajwa tena leo Jumatatu Mei 11,2020 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Shinyanga na kuahirishwa hadi Mei 25, 2020 itakapotajwa tena kwa ajili ya maombi ya dhamana.

Katika mashtaka 12 ya uhujumu uchumi anayokabiliwa nayo Mbunge huyo ni pamoja na shtaka la kwanza, tatu ambayo ni kupatikana na silaha, shtaka la pili ni kupatikana na risasi, la nne ni kumiliki silaha aina ya Riffle kinyume na sheria kwa mujibu wa Sheria ya kumiliki silaha Na. 2 ya mwaka 2015, shtaka la tano, sita, saba, nane na tisa ni kumiliki risasi bila kibali, shtaka la 10 ni kumiliki silaha bila kibali na 11 ni kumiliki risasi isivyo halali.

Mbunge huyo alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Mei 8, 2020 mahakamani hapo katika shauri la uhujumu uchumi namba 10 la mwaka 2020 na kusomewa mashitaka 12 ya uhujumu uchumi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Ushindi Swalo. 

Upande wa mshtakiwa ukiongozwa na Wakili Frank Mwalongo uliomba mteja wao apate dhamana lakini maombi yao yalishindikana baada ya upande wa Mashitaka ukiongozwa na Mkuu wa Mashtaka mkoa wa Shinyanga, Margareth Ndaweka kupinga na kueleza kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa dhamana hiyo ambapo Hakimu Swalo alikubaliana na hoja hiyo na kuahirisha shauri hilo hadi Mei 25, mwaka huu ambapo litaletwa kwa ajili ya kutajwa tena na kushughulikia dhamana, ambapo mshtakiwa amerudishwa tena rumande.

Wakili wa mshtakiwa, Frank Mwalongo amewaeleza waandishi wa habari kuwa mteja wake amekosa dhamana kwa kuwa hati ya mashtaka haijataja thamani (kiasi) anachodaiwa kuhujumu mshtakiwa, hivyo haina mamlaka ya kutoa dhamana na kuwataka waombe mahakama kuu ambayo ina mamlaka ya kutoa dhamana hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527