THBUB YASIKITISHWA NA TAARIFA YA VITENDO VYA BAADHI YA MADAKTARI NA WAUGUZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA, MWANANYAMALA KUWANYANYAPAA NA KUWASUMBUA WAGONJWA

Kusikitishwa na taarifa ya vitendo vya baadhi ya Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala kuwanyanyapaa na kuwasumbua Wagonjwa
____________________


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa na taarifa ya vitendo vinavyofanywa na baadhi ya Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala vya kuwanyanyapaa na kuwasumbua wagonjwa wanaoenda kupata matibabu kwa kuwataka wagonjwa hao kwenda kufanya vipimo vya Korona kabla ya kuanza kupata matibabu.

Tume imesikitishwa na jambo hilo kwa sababu kila mwananchi ana haki ya kufurahia haki ya afya kwa kupata matibabu mazuri na ya uhakika. Madaktari na Wauguzi wanapaswa kutambua kuwa sio kila Mgonjwa ana maambukizi ya Korona.

Tume inaamini vitendo vya namna hiyo ni ukiukwaji wa haki ya afya kwa wananchi, na vinaweza kusababisha wagonjwa kupoteza maisha.

Aidha, Tume inatoa pongezi nyingi kwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa  Ummy Mwalimu kwa kuchukua hatua za haraka za kukemea vitendo hivyo vya baadhi ya Madaktari na Wauguzi ambavyo vinaweza kuchafua taswira nzuri ya sekta ya Afya na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali.

Hata hivyo, Tume inaiomba  Serikali iendelee kuhakikisha hospitali zinaendelea kutoa huduma nzuri kwa Wagonjwa ili kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima.

Mwisho, Tume inaiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya Madaktari na Wauguzi ili  kuvitafutia ufumbuzi wa haraka.


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527