MWENYEKITI BAVICHA KILIMANJARO KORTINI KWA KUCHAPISHA PICHA ZA NGONO

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), Mkoa wa Kilimanjaro, Lemrus Mchome (30), amefikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma za kusambaza nyaraka za ngono ikiwamo picha na video kwa nia ya kuleta ashki za ngono kinyume cha sheria.


Mchome ambaye ni mkazi wa Kisaranga, Wilaya ya Mwanga, amesomewa mashtaka yake katika Mahakama ya Hakimu Kisutu, jijini Dar es Salaam iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo.

Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kuweka, alidai kuwa kati ya Januari Mosi na Aprili 30, mwaka huu, jijini Dar es Salaam mshtakiwa alitenda kosa la kusambaza nyaraka za ngono.

Kweka aliendelea kudai kuwa Mchome alisambaza nyaraka za ngono ikiwamo picha na video za mwanamume kupitia simu yake ya mkononi kwa nia ya kuleta ashki za ngono kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo, Kweka aliiomba mahakama isitoe dhamana kwa mshtakiwa huyo kwa sababu upelelezi unaendelea.

Mchome alidai mashtaka hayo yamemshtua kwa kuwa alikamatwa Mei 11, mwaka huu, lakini amezuiliwa kuonana na ndugu zake pamoja na wanasheria.

Alidai kesi hiyo sio ya kwanza kwa mahakama hiyo kwa kuwa zipo ambazo zilitolewa dhamana huku upelelezi ukiendelea.

Akijibu hoja hiyo, Kweka alidai huo ni mkakati wao wa kuendelea na upelelezi.

Hakimu Mwaikambo alisema uamuzi wa mabishano ya pande zote mbili kuhusu dhamana itatolewa Juni 2, mwaka huu, mshtakiwa arudishwe mahabusu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post