KAMPUNI YA EVERWELL CABLE AND ENGINEERING CO. LTD YACHANGIA SH. MILIONI 100 KUKABILIANA NA CORONA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana, na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb), amepokea msaada wa hundi yenye thamani ya sh. milioni 100 iliyotolewa na kampuni ya Everwell Cable and Engineering Co. Ltd, inayojishughulisha na uzalishaji wa nyaya za kusafirisha umeme kwenye miradi mbalimbali ya umeme hapa nchini, kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID- 19).

Waziri amepokea mchango huo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa  tarehe 13 Mei, 2020 katika Ofisi ya Waziri Mkuu Mlimwa, Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kupokea mchango huo Waziri Mhagama ameipongeza kampuni hiyo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha inapambana na janga la ugonjwa wa COVID-19. 

“Kwa niaba ya serikali nawashukuru sana kwa kuwa sehemu ya watanzania katika kipindi hiki cha mapambano ya janga la COVID-19. Tunawashukuru sana kwa kuendelea kuwa sehemu ya shida na raha za Taifa hili,” ameeleza Waziri Mhagama. 

Aidha, Waziri Mhagama amewahakikishia watanzania kuwa michango hiyo inasimamiwa vyema na serikali kwa kuitumia michango hiyo katika kushughulikia majukumu yaliyopangwa ya kupambana na janga la ugonjwa wa COVID-19. 

Awali, Waziri wa Nishati Dkt. Medadi Kalemani ameipongeza kampuni hiyo kwa mchango wao kwa Serikali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.
“Kampuni hii ni moja ya wawekezaji waliojenga Kiwanda hapa nchini, lakini pamoja na shughuli za uwekezaji wameguswa katika kipindi hiki wakati serikali inapambana na
janga hili la ugonjwa wa COVID-19, tunawashukuru sana kwa mchango wenu kwa watanzania ”amesema Dkt. Kalemani. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Everwell Cable and Engineering Co. Ltd, Bw. Jiaopeng Lu ameeleza kuwa Kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na watanzania katika uzalishaji wa bidhaa za kiwanda kabla ya Janga hili la Ugonjwa wa COVID-19, hivyo hawana budi kuhakikisha watanzania wanakuwa salama ili waendelee kushirikiana nao katika shughuli za uzalishaji. 

IMETOLEWA NA: 
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI 
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post