WATATU MBARONI KWA KUDAKWA NA MTAMBO WA KUTENGENEZEA GONGO...YUMO MWANAFUNZI WA DARASA LA 6


Picha haihusiani na habari hapa chini

Jeshi la Polisi mkoani Rukwa, linawashikilia watu watatu akiwamo mwanafunzi wa darasa la sita kwa tuhuma za kukutwa na mtambo wa kutengenezea pombe haramu aina ya gongo, pamoja na lita 20 za pombe hiyo.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 19 ni wa Shule ya Msingi Katusa katika Manispaa ya Sumbawanga.

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Justine Masejo, alisema kuwa watu hao wamekamatwa kufuatia operesheni maalumu iliyoongozwa na mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoani Rukwa, Ralph Meela pamoja na maofisa wa polisi na askari.

Kabla ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, alisema Jeshi la Polisi lilipata taarifa kuwa kuna watu katika kitongoji cha Katusa Manispaa ya Sumbawanga wanafanya biashara haramu ya kuuza gongo, kitendo kinachosababisha mkusanyiko wa watu wanaokunywa pombe hiyo bila kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizo ya ugonjwa wa Covid-19.

Kamanda huyo alisema baada ya taarifa hizo ndipo askari polisi wakiongozwa na Meela walivamia katika eneo hilo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa katika eneo la tukio, huku baadhi yao wakiwa wanakunywa pombe hiyo, akiwamo mwanafunzi huyo.

“Baada ya kuwakamata watuhumiwa hao, polisi walibaini kuwa licha ya kutenda kosa la kuuza na kunywa pombe hiyo haramu, hawakuwa wanachukua tahadhari yoyote ya kujikinga kuambukizo ya virusi vya corona kwa kuwa walikuwa katika mkusanyiko..hakuna hata aliyevaa barakoa wala hakuna maji ya kunawa mikono, pia hakuna kitakasa mikono cha aina yoyote,” alisema. 

Kamanda Masejo alisema watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527