FISI AUA MTOTO WA MIAKA MITATU AKICHEZA NA WENZAKE KISHAPU


Kamanda wa polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog 
Mtoto aitwaye Sungwa Kulwa mwenye umri wa miaka mitatu (03) mkazi wa kijiji cha Dodoma Kata ya Masanga, wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga amefariki dunia baada ya kushambuliwa na fisi sehemu za kichwani wakati akicheza na wenzake nje ya nyumba yao. 

Kamanda wa polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea jana Aprili 30,2020 majira ya saa moja usiku katika kijiji cha Dodoma Kata ya Masanga, Wilaya ya Kishapu

“Mtoto huyo alikuwa akicheza na watoto wenzake nje ya nyumba yao umbali wa mita kumi, ndipo fisi huyo alitokea kwa ghafla kutoka vichakani na kumshambulia kisha kumburuza umbali wa mita 100 ambapo alimuachia baada ya kusikia kelele za wananchi waliokuwa wakimfukuza”,ameeleza Kamanda Magiligimba. 

Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wako mazingira salama muda wote, wasiachwe peke yao na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari hasa kwa kipindi hiki ambacho fisi wamekuwa wakionekana maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post