WABUNGE WA CHADEMA WAKIUKA MAAGIZO YA MWENYEKITI WAO FREEMAN MBOWE YA KUTOHUDHURIA BUNGENI


Wabunge wanane wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana walikaidi maagizo ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kuwataka kutohudhuria vikao vya bunge na kujitenga kwa siku 14.

Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Joseph Selasini (Rombo), Peter Lijualikali (Kilombero), David Silinde (Momba), Antony Komu (Moshi Vijijini), Susan Masele (Viti Maalum), Jaffary Michael (Moshi Mjini), Latifa Chande na Subrina Sungura (Viti Maalum).

Wabunge hao walihudhuria mkutano wa 18 wa kikao cha 21 cha Bunge la 11, kilichojadili na kupitisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na walikuwa katika ukumbi wa Msekwa na ukumbi mkuu wa Bunge.

Mbunge Selasini wiki iliyopita alilalamika bungeni kwa kuondolewa kwenye kundi songezi la wabunge wa Chadema na kushindwa kuchangia mjadala wowote tangu kuanza kwa bunge, hadi alipopitia kwa Spika, Job Ndugai.

Aidha, siku iliyofuata Selasini alitangaza kuendelea kuwa mbunge, lakini hana mpango wa kugombea kupitia Chadema, bali NCCR- Mageuzi, Oktoba mwaka huu.

Februari mwaka huu, Komu alitangaza kuwa atagombea ubunge jimbo hilo, na kwamba wakati ukifika atagombea kupitia NCCR- Mageuzi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post