ALGERIA YAFUNGA TENA BIASHARA KWA HOFU YA CORONA BAADA YA TARATIBU KUKIUKWA


Biashara nyingi nchini Algeria zilizokuwa zimefunguliwa wiki iliyopita, zimefungwa tena, katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo, kwa sababu ya kutofuata kanuni za usafi na hatua ya kutokaribiana kwa umbali wa mita moja.

Tangu kuanza kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani zaidi ya wakuu 15 wa majimbo kati ya 48 wamejikuta hatua walizochukua kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona hazitekelezwi na wafanyabiasha pamoja na raia katika majimbo yao, na hivyo kuagiza kufungwa kwa biashara zote.

Maeneo yaliyohusishwa zaidi na uamuzi huo ni maduka ya nguo, maduka ya viatu, migahawa na maduka ya mikate, yanayotembelewa sana wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, pamoja na maduka ya manukato.

Picha za milolongo ya watu wakiwa mbele ya maduka zimewakasirisha sana viongozi na maafisa wa afya nchini Algeria ambao wamesikitishwa na hatua ya wananchi ya kutoheshimu kanuni na taratibu za kuzuia maambukizo ya virusi vya Corona.

Ijumaa iliyopita, Rais Abdelmadjid Tebboune wa nchi hiyo alitishia kuongeza masharti ya raia kutotembea ikiwa hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona zitapuuziwa na kutotekelezwa ipasavyo.

Vifo 463 vimerekodiwa nchini Algeria tangu kuripotiwa kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya Corona, Februari 25, kulingana na kamati ya kisayansi inayofuatilia jinsi ugonjwa huo unavyoendelea nchini.

Algeria inashika nafasi ya nne kwa idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya Corona barani ya Afrika baada ya kuthitisha kesi 4,474 hadi sasa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post