Picha : SHIRIKA LA AGAPE ACP LATUA VIJIJINI KUTOA ELIMU YA UKATILI WA KIJINSIA NA CORONA


Shirika la AGAPE ACP ambalo linatetea haki za watoto mkoani Shinyanga, limetoa elimu ya ukatili wa Kijinsia na jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, kwa wajumbe wa kamati ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (Shinyanga Vijijini).


Elimu hiyo imetolewa leo Mei 22, 2020 katika ofisi ya Kata ya Mwamala kwa kukutana na wajumbe wa MTAKUWWA Kata  ya Mwamala.


Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE ACP John Myola, amesema katika kipindi hiki cha janga la Corona, wameamua kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi hayo sambamba na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwa ufadhili wa Shirika la Mundo Cooparante.


Amesema Shirika hilo kwa kushirikiana na wataalamu wa afya wanatoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona katika maeneo ya vijijini pamoja na elimu ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili jamii ibaki kuwa salama.


"Shirika letu la AGAPE tunaungana na Serikali kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, pamoja na kupinga matukio ya ukatili katika maeneo ya vijijini, na sasa tupo Kata ya Mwamala ambapo pia tumetoa vifaa vya kujikinga na maambukizi hayo zikiwamo ndoo za maji tiririka na sabuni," amesema Myola.


Naye Afisa maendeleo Kata ya Mwamala Sophia Philbert, ambaye pia ni katibu wa MTAKUWWA amewataka wajumbe hao kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi katika kutoa elimu ya kujikinga na virusi vya Corona, pamoja kuimarisha ulinzi dhidi ya watoto na kuwazuia kuzurura hovyo.

Kwa upande wake Mhudumu wa afya katika kituo cha Samuye, Ilambona Alfred, ametoa elimu kwa wajumbe hao namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka, kukaa umbali wa mita moja, kuvaa barakoa, pamoja na kuepuka mikusanyiko.


Aidha afisa tarafa wa Samuye Ntarle Magese, ametoa wito kwa wananchi kuacha kupuuzia janga hilo la maambukizi ya virusi vya Corona licha ya maambukizi kupungua, bali waendelee kuchukua tahadhari hadi pale Serikali itakapo tangaza janga hilo limeisha hapa nchini.




TAZAMA PICHA HAPA CHINI

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE ACP John Myola, akitoa elimu ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga leo Ijumaa Mei 22,2020. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE ACP John Myola akiendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili kwa wajumbe wa Kamati ya Mtakuwwa Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Afisa Maendeleo Kata ya Mwamala Sophia Philbert, ambaye pia ni Katibu wa MTAKUWWA, akitoa elimu kwa wajumbe wa Kamati ya MTAKUWWA namna ya kutekeleza majukumu yao katika kupambana kupunguza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Mhudumu wa afya kutoka Kituo cha Afya Samuye Ilambona Alfred, akitoa elimu namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Afisa tarafa ya Samuye Ntarle Magese, akisisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona licha ya kupungua.

Diwani wa kata ya Mwamala Hamisi, akipongeza Shirika la Agape kwa kuendelea kuhudumia jamii kwa kutoa elimu ya Corona pamoja na vifaa sanjari na elimu ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Afisa Mradi wa Kutokomeza ndoa za utotoni na kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto kutoka Shirika la AGAPE ACP Sophia Rwazo, akiwasihi wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA Mwamala, wachape kazi kwa kushirikiana ili waweze kutimiza malengo ya kupunguza ukatili ndani ya jamii.

Wajumbe wa MTAKUWWA Mwamala wakiwa kwenye kikao.

Wajumbe wakiendelea na kikao.

Mjumbe wa Kamati ya MTAKUWWA Salome Ndaki akichangia mada.

Mjumbe wa kamati ya MTAKUWWA Boniphace Boazi akichangia mada.

Mjumbe wa kamati ya MTAKUWWA Ramadhani Dotto akichangia mada.

Mratibu wa Miradi kutokana Shirika la AGAPE Peter Amani akishusha vifaa vya kujikinga na virusi vya Corona tayari kwa kuvigawa katika kata ya Mwamala.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE ACP John Myola, akitoa elimu namna ya kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona kwa wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA kabla ya kuvigawa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE ACP John Myola, (wa kwanza kulia), akitoa maelezo wakati wa kukabidhi kifaa cha kisasa cha kunawa mikono kwa sabuni na maji tirika kwa wajumbe wa MTAKUWWA ambacho kitawekwa kwenye kituo cha afya Bogogo ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Zoezi la kugawa vifaa vya kisasa ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona likiendelea, ambapo kifaa hicho kitapelekwa kituo cha afya Mwamala.

Zoezi la kupokea vifaa vya kisasa ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona likiendelea, ambapo kifaa hicho kitawekwa kwenye ofisi ya Kata ya Mwamala.

Diwani wa Kata ya Mwamala Hamisi Masanja akinawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara baada ya kukabidhiwa kifaa hicho na Shirika la AGAPE ACP kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Afisa mtendaji wa Kata ya Mwamala Suzani Kayange, akinawa mikono kwa sabuni na maji tirika mara baada ya kukabidhiwa kifaa cha kisasa na Shirika la AGAPE ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, kulia ni mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE ACP John Myola.

Afisa tarafa Samuye Ntarle Magese akinawa mikono kwa sabuni na maji tiririka.

Sheikhe Ramadhani Dotto,akinawa mikono kwa sabuni na maji tiririka.

Picha zote na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527