WHO: AFRIKA HAITAKUWA UWANJA WA KUFANYIA MAJARIBIO CHANJO YA CORONA


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amekosoa vikali matamshi ya kibaguzi ya madaktari wawili wa Ufaransa waliopendekeza kufanyia majaribio chanjo ya corona barani Afrika.

Dakta Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, "Afrika haiwezi na wala haitofanywa uwanja wa majaribio ya chanjo yoyote ya Covid-19. 

WHO itafuata kanuni zote na kufanya majaribio ya chanjo yoyote au matibabu duniani kote, bila kujali ni Ulaya, Afrika au pahala popote pale.

Matamshi ya madaktari hao waliyoyatoa kwenye mjadala wa runinga yamezua ghadhabu, na wametuhumiwa kwa kuwachukulia Waafrika kama "nguruwe wa kufanyiwa majaribio ya maabara".

Mkurugenzi Mkuu wa WHO ameonekana kuongea na ghadhabu kwenye kikao na waandishi wa habari mjini Geneva ameeleza bayana kuwa, matamshi ya wanasayansi hao wa Kifaransa katika karne hii ya 21 ni ya kibaguzi, ya kufedhehesha, na yanayoashiria mabaki ya fikra za kikoloni.

Viongozi wa nchi za Afrika wameendelea kukosoa matamshi ya madaktari hao wakubwa wa Ufaransa, Camille Locht na Jean-Paul Mira, ambao hivi karibuni katika kipindi cha runinga, walipendekeza kwa kejeli na dharau kufanyika majaribio hayo ya chanjo ya corona barani Afrika.

Siku chache zilizopita, wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walikosoa vikali mpango huo wa kufanyia majaribio chanjo ya corona nchini humo ambao serikali ya Kinshasa imeafiki wakisisitiza kuwa, ni fedheha kwa serikali kuruhusu taifa hilo ligeuzwe 'panya wa maabara'.
Afrika hadi saa imeripoti kesi elfu 10 pekee

Hii ni baada ya Jean-Jacques Muyembe, Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Biolojia anayeongoza jopokazi la kupambana na janga la corona nchini DRC kusema kuwa, "tumeteuliwa kufanya majaribio haya. Chanjo hiyo itazalishwa Marekani, Canada au China. Utafika wakati fulani ambapo itashindikana kudhibiti virusi vya corona, njia pekee ya kuidhibiti ni chanjo. Chanjo ndiyo iliyotusaidia kudhibiti Ebola."

Pendekezo hilo la Wamagharibi la kuwageuza Waafrika 'panya wa maabara' linakuja katika hali ambayo, aghalabu ya makumi ya maelfu ya vifo na kesi zaidi ya milioni moja na laki tatu za ugonjwa wa Covid-19 (corona) zimeripotiwa katika nchi za Ulaya na Marekani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post