MWANAFUNZI AFARIKI DUNIA KWA KUNASWA UMEME JUU YA MTI


Mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Mrunyigo, Kijiji cha Kiemba mkoani hapa, Calvin Eranga (14) , amefariki dunia baada ya kunaswa akiwa amepanda juu ya mti uliokuwa umegusana na nyaya za umeme.

Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco), Mkoa wa Mara, Meshak Laurent, akizungumzia tukio hilo alisema, mwanafunzi huyo alifikwa na mauti mwishoni mwa wiki baada ya kupanda juu ya mti ambao ulikuwa jirani na nguzo zenye nyaya za umeme.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa, elimu kwa wananchi ya kuchukua tahadhari na kulinda miundombinu inatolewa kwa umma, lakini shughuli za kibinadamu na uzalishaji zinaendelea kandokando ya njia za umeme licha ya tahadhari kutolewa mara kwa mara.

Alisema ni jukumu la jamii wakiwamo viongozi wa serikali na kijamii kushirikiana kuhifadhi miuondombinu ikiwamo ukataji miti iliyopadwa jirani na njia za umeme kutokana na kutoruhusiwa kuikata isipokuwa Tanesco. 

Baba mkubwa wa marehemu, Katekista Leo Ekingo, alisema mwanafunzi huyo alipanda katika mti wa mchongoma ambao ulikuwa unagusana na nyaya za umeme na kusababisha kifo chake.

“Miti ilikuwa inagusana na nyaya za umeme, kijana akiwa juu ya mti wa mchongoma akanaswa na akawa ananing’inia kwa muda kisha umeme ukamwachia akadondoka chini na kufariki dunia…,” alisema.

Ofisa wa Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za nishati na maji (Ewura CCC), Mkoa wa Mara, Dennis Ndanu, alisema ofisi za baraza hilo limepata taarifa ya kifo cha mwanafunzi huyo na linafuatilia ili kuhakikisha haki na stahiki za muathirika zinapatikana kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post