WALIOAMBUKIZWA VIRUSI VYA CORONA AFRIKA WAFIKA 10,692


Watu wengine 535 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona barani Afrika na kuifanya idadi ya watu wenye ugonjwa wa COVID-19 katika nchi 52 za bara hili kufikia 10,692.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) ambayo pia imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Misri ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuripoti kesi za ugonjwa wa COVID-19 mwezi Februari na tokea wakati huo ugonjwa huo umeenea kwa kasi katika wiki za hivi karibuni.

Katika taarifa, Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO barani Afrika amesema ugonjwa wa COVID-19 si tu kuwa unaweza kusababisha vifo vya maelfu ya watu bali pia unaweza kusababisha janga la kiuchumi na kijamii. 

Ametahadharisha kuwa iwapo ugonjwa wa corona utaenea nje ya miji barani Afrika basi itakuwa changamoto kubwa kwa bara hilo.

Moeti amesema kuna haja ya kuziwezesha jamii mashinani kwa kuzingatia mazingira ya kila eneo. 

Aidha amesema WHO inafanya kazi kwa pamoja na serikali za Afrika ili kuimarisha kiwango cha upimaji, karantini, kuwafuatilia wale waliokutana na walioambukizwa, kuzuia maambukizi zaidi na kujumuisha jamii katika kuzuia kuena ugonjwa huo.

-Parstoday


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527