RC MTAKA : TUSHEREHEKEE PASAKA TUKICHUKUA TAHADHARI DHIDI YA CORONA

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka leo ameshiriki ibada ya Pasaka katika makanisa tofauti mjini Bariadi na kuwasisitiza waumini na wananchi wote wa Mkoa wa Simiyu kutulia, kuepuka safari zisizo za lazima na kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Serikali.

Mtaka ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akitoa salamu za Pasaka za Mkoa aliposhiriki ibada katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu John, Parokia ya Mtakatifu Luka, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Bariadi Mjini na Kanisa la Africa Inland Church of Tanzania (AICT) leo Aprili 12, 2020.

“Nimeona watu wananawa mikono utaratibu huu usiishie kwenye nyumba za ibada na maeneo ya kutolea huduma, uende mpaka nyumbani,tunapokuwa kwenye nyumba za ibada pia tuzingatie umbali katika ukaaji wetu na wakati wa kupokea huduma za kiroho: pasaka hii tutulie majumbani tuepuke safari zisizo lazima na tufuate maelekezo ya Serikali.” alisema Mtaka.

Aidha, pamoja na kuwasisitiza wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima Mtaka ametoa wito kwa jamii kuona namna ya kuwasaidia zaidi wazee, watoto  na watu wenye magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu kuepuka zaidi mikusanyiko hiyo ili kuwaondolea hatari ya kupata maambukizi kutokana na hali ya kinga zao za mwili.

Katika hatua nyingine Mtaka amewataka wazazi kuwasimamia watoto wao kujisomea kwa bidii kipindi hiki ambacho shule zimefungwa kutokana na tahadhari ya maambukizi ya Virusi vya Corona hususani wale wa madarasa ya Mitihani ya Kitaifa kwa kuwa mitihani hiyo bado ipo na itafanyika.

Sambamba na hayo Mtaka amewaasa wananchi wa Mkoa wa Simiyu kutunza chakula ambacho kimepatikana mwaka huu na kutokiuza kwa matumizi ambayo si ya lazima hususani katika kipindi hiki ambacho chakula kinauzwa kwa bei ya chini huku akiwasisitiza kujiunga na Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii ili waweze kupata unafuu katika huduma za matibabu.

Kwa upande wao viongozi wa makanisa akiwemo Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu John, Peter Mkunya, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Luka, Martine Jilala, Mchungaji wa KKKT Bariadi, Greyson Kinyaha na Mchungaji wa AICT, Amosi Ndaki wamesema wametumia Maadhimisho ya Kufufuka kwa Yesu Kristo(Pasaka) kuliombea Taifa ili Mungu aliponye na Janga la Corona na kuendelea kuwakumbusha waumini kuzingatia maelekezo ya viongozi wa Serikali na wataalam wa afya.

Koga Mihama na George Lyimo ni miongoni mwa waumini waliohudhuria ibada ya pasaka wameishukuru Serikali kwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa kujikinga na Maambukizi ya CORONA huku wakitoa wito kwa wananchi wote kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali ili Maambukizi ya Virusi vya Corona yaishe nchini Tanzania.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post