ASP SWEBE : TUENDELEE KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA CORONA

Na WAMJW- DSM

Mrakibu mwandamizi wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam ASP Swebe ametoa wito kwa wananchi, hususan Wana Dar es Salaam kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Ameyasema hayo wakati akiwa katika majukumu yake ya ukaguzi wa namna gani kituo cha Polisi Pangani kilichopo Ilala Jijini Dar es Salaam kimechukua hatua ya kukabiliana dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

“Tunaendelea kukumbusha Wananchi wa hususan Wanaotoka Jijini Dar es Salaam kunawa mikono na kuchukua hatua zote za tahadhari zinazotakiwa, tunaendelea kusisitiza kila mmoja katika familia yake aendelee kuchukua hatua ambazo Wizara ya Afya inapendekeza” alisema

Kwa upande mwingine, ASP Swebe ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuja na kampeni ya “Mikono safi, Tanzania salama” inayohamasisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, hali inayoonesha jinsi gani Serikali imewekeza kwenye Afya ya wananchi.

“Kwanza nitoe shukrani kwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa Kampeni inayoendelea ya “Mikono safi, Tanzania salama”, hii inaonesha ni jinsi gani Serikali imewekeza kwenye Afya ya wananchi” alisema.

Aidha, ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuendelea kulisaidia Jeshi la polisi vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona ikiwemo vitakasa mikono na Barakoa (mask).

Kwa upande wake, Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine Ngowi, amewataka madereva wote wa vyombo vya moto hususan bodaboda na bajaj kuhakikisha wanavitakasa vyombo vyao vya usafiri kwa sabuni mara kwa mara ili kuua maambukizi ya virusi vya Corona endapo vitakuwepo.

Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527