CHAMA CHA WALIMU IRAMBA MKOANI SINGIDA CHAPATA VIONGOZI WAPYA


Viongozi wapya wa Chama cha Walimu nchini (CWT) Wilaya ya Iramba wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuchaguliwa kupitia mkutano mkuu uliofanyika jana.


Na Godwin Myovela, Singida

WAJUMBE wa Chama cha Walimu nchini (CWT) Wilaya ya Iramba, mkoani hapa kupitia mkutano mkuu wamefanya mabadiliko ya safu ya juu ya uongozi wake kwa kumchagua Anania Mbuta kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho, huku aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Hamis Kumara kujikuta akipata kura pungufu.

Pia kupitia mkutano huo wa uchaguzi, wajumbe waliamua kumwondoa madarakani aliyekuwa mwekahazina wa muda mrefu wa chama hicho William Gunda, na nafasi yake kuchukuliwa na Sebastian Gunda-huku nafasi ya Mwenyekiti wa Kitengo cha Walimu Wanawake (KE) akikakabidhiwa Dorcus Mungulu.

Katika uchaguzi huo wa kikatiba uliofanyika jana kwenye ukumbi wa halmashauri wilayani hapa, na kusimamiwa na Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Singida, Aran Jumbe, jumla ya wajumbe takribani 120 ambao wanawakilisha zaidi ya walimu 1200 walishiriki na kuwa sehemu ya mabadiliko hayo.

“Nawashukuru wajumbe kwa kuniamini na kunikabidhi jukumu hili la kuhakikisha haki na maslahi ya walimu vinazingatiwa kwa vitendo na kwa wakati, timu yote ya uongozi mliyonipa iko vizuri, nawahakikishia tutachapa kazi sintawaangusha,” alisema Mwenyekiti mpya Mbuta.

Aidha, wajumbe wengine waliochaguliwa kupitia mkutano huo uliokuwa na mvutano mkali baina ya wagombea ni pamoja na Grace Shirima ambaye ameshinda kwa nafasi ya mwekahazina Kitengo cha Wanawake, huku Damiano Awali akiaminiwa kushika nafasi ya uwakilishi wa Taasisi na Uongozi.

Hata hivyo, nafasi ya uwakilishi nafasi ya chuo alipewa Thomas Sekenga, na uwakilishi wa wenye Ulemavu ukienda kwa Emanuel Suwi, huku Vijana nao wakimpata mwakilishi wao Griflin Kaleshu. Ushindi wa nafasi ya uwakilishi wa cwt kwa walimu wanawake wilayani hapa hatimaye umekwenda kwa Veleriana Masangya.

Walimu wanne ambao ni Clemensi Pegia, Makilagi Makalanga, Godfrey Athuman na Elia Sumbi wamechaguliwa kuwakilisha walimu wa Shule za Msingi, huku walimu wawili Seaclif Msagaha na mwenzake Magreth Gregory wao watawakilisha walimu wa shule za sekondari .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527