TULONGE AFYA YAZINDUA KIPINDI CHA 'WASHA KIDEO NA SITETEREKI' LIVE MTANDAONI KUELIMISHA VIJANA MASUALA YA AFYA 'COVID- 19'


Ili kukabiliana na changamoto za COVID-19 ambazo zimeathiri shughuli mbali mbali Nchini Tanzania, Programu ya USAID Tulonge Afya imezindua kipindi maalum cha TV cha moja kwa moja (yaani live) "Washa Kideo na Sitetereki" kipindi ambacho pia kitakuwa kikirushwa moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii. 


Malengo ya kipindi hiki cha Washa Kideo na SITETEREKI ni kushughulikia changamoto za kiafya zinazohusiana na vijana na jinsi wanavyoweza kukabiliana nazo katika kipindi hiki cha janga la COVID-19 ambapo mifumo yote ya kila siku imevurugika kwani watu wote wanahimizwa kukaa nyumbani.

Programu ya SITETEREKI ni jukwaa la kubadilisha tabia na mienendo ya kila siku (SBC) linalolenga vijana. Jukwaa hili linasaidia kukuza Muingiliano wa vijana nchini Tanzania ili kujua vyema, kuhamasisha, na kuwezesha vijana kuchukua tabia njema ambazo zitaboresha ustawi wao kwa jumla. SITETEREKI imeundwa kusaidia moja kwa moja vipaumbele vya kimkakati kwa vijana katika Serikali ya Tanzania na inafadhiliwa na serikali ya Marekani kupitia USAID.

Akizungumza leo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, Mkurugenzi wa USAID nchini Tanzania Andy Karas alisema kuwa kipindi cha Washa Kideo na SITETEREKI kimebuniwa kusaidia vipaumbele vyaSerikali ya Tanzania kwa Vijana.. 'Sote tunaelewa kuwa sasa vijana wetu hawawezi kwenda tena kwenye mikusanyiko ya kijamii, Luninga pamoja na mitandao ya kijamii sasa imekuwa ndio kimbilio la vijana wengi.

 Kwa sababu ya idadi kubwa ya watu wanaokaa nyumbani kwa sasa, utumiaji wa vyombo vya habari na hasa Luninga pia umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Vijana wetu wamekuwa wakivutiwa na mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na YouTube, Instagram, pamoja na vyombo vingine vya habari vinapokuwa vikirusha taarifa zao moja kwa moja. 

Kwa sababu hiyo, tumezindua kipindi "Washa Kideo na SITETEREKI" ili kutoa fursa ya kipekee ya kufikia mamilioni ya vijana wa kitanzania kwa njia ambayo huwashawishi wakati wa kutoa ujumbe muhimu wa afya ili kuwasaidia kuwalinda wao na familia zao, na nchi kwa ujumla kwa wakati wote na janga la COVID-19. "Karas alisema.

Aliongeza, ‘COVID-19 inajaribu kutikisa mienendo yetu ya maisha lakini kupitia muendelezo wa ufadhili wa serikali ya Marekani na uwekezaji wake katika afya ya Watanzania na taasisi za afya, na kuwa na mienendo mizuri ya kiafya ambayo tunashirikiana pamoja leo hii, vijana wa Kitanzania “hawata - tetereka”. 

Serikali ya Marekani inaendelea kusaidia kupambana na mlipuko wa COVID-19 kwa kuchukua hatua za haraka kupitia taasisi zake mbalimbali hapa nchini. Serikali ya Marekani inashirikiana na wafanyakazi wa Tanzania walio mstari wa mbele katika kupunguza maambukizi, kutoa huduma kwa waathirika, na kuandaa jamii kwa kutoa vifaa muhimu vinavyohitajika kupambana na COVID-19.

Akizungumza kuhusu kipindi cha Washa Kideo na SITETEREKI, Mkurugenzi wa Miradi Tulonge Afya Waziri Nyoni alisema kuwa Kipindi hicho Kina lenga kufikia vijana zaidi ya milioni 20 wenye umri kati ya miaka 14 mpaka 25 hapa nchini.

Tamasha hilo litaunga mkono juhudi za kupambana na janga hatari la COVID-19, na VVU, afya ya uzazi na malengo ya mkakati wa uzazi pamoja na kukuza tabia chanya kwa vijana.

‘Tamasha la Washa Kideo na SITETEREKI litakuwa likirushwa kila Ijumaa kwa masaa mawili kuanzia saa tatu mpaka saa tano usiku huku wasanii wakitumbuiza moja kwa moja kupitia Clouds TV na Clouds Radio. Vile vile, litakuwa likirusha moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii ya Clouds Media. Wasanii, ma DJ pamoja na waendesha kipindi hicho pia watakuwa wakirusha moja kwa moja kwenye mitandao yao ya kijamii na hivyo kuweza kuwafikia zaidi ya wafuasi wao milioni 22.4 kwenye mtandao wa Instagram. Watazamaji wataweza kuwasiliana moja kwa moja na wasanii’ Nyoni alisema.

Tamasha la kipindi cha Washa Kideo na SITETEREKI litawaleta pamoja wasanii mbali mbali ikiwa ni pamoja na Maua Sama, jux na G-Nako, pia watakaoshiriki kwa njia ya mtandao watakuwa Harmonize, Nandy, Dogo Janja na Nikki wa Pili. Aliongeza kuwa watangazaji wa programu hiyo watakuwa Nickson George na Mina Ally wakati DJ’s watakuwa DJ D-Omy na DJ Sinyorita.

Mradi wa Tulonge Afya, ni mradi wa miaka 5 unaofadhiliwa na shirika la Marekani la USAID, miradi ya Tulonge afya ina lengo la kukuza shughuli chanya za afya katika kaya na jamii nchini Tanzania huku ikilenga wanawake na vijana. Mradi wa Tulonge Afya unatekelezwa na FHI 360 Wizara ya Afya , Maendeleo ya Kijamii, Wazee na Watoto pamoja na washirika wengine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post