SERIKALI YAONGEZA TIJA NIC KWA KUKOMESHA UBADHIRIFU

Na. Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, amesema hakuna ubadhirifu unaoendelea katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) baada ya Serikali kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kubadili uongozi wa Shirika hilo pamoja na kuimarisha mifumo yake ya ukusanyaji mapato.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Dkt. Kijaji, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ubungo. Mhe. Saed Kubenea, aliyetaka kujua ukweli kuhusu kuendelea kwa ubadhirifu katika Shirika la NIC na mpango wa Serikali wa kulisaidia shirika hilo kukabiliana na ushindani wa kibiashara.

Alisema kuwa hivi sasa Shirika hilo linatumia Mfumo wa Ukusanyaji Mapato ya Serikali (GePG) hatua iliyoimarisha mapato yake pamoja na kuanza kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kufanya malipo yake yote badala ya kutumia Hundi.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Shirika la NIC lilianza kutumia Mfumo wa Makusanyo ya Mapato ya Serikali kuanzia Novemba, 2019 na kuondoa ukusanyaji wa mapato kwa fedha taslimu pamoja na kuongeza udhibiti katika ulipaji wa madai ikiwemo kufanya ukaguzi maalum wa madai yote ya bima za maisha ili kujiridhisha kuhusu uhalali wake.

Alisema Matumizi ya Hundi (cheque) yamesitishwa kuanzia Desemba, 2019 katika malipo yake yote na kuanza kutumia mfumo wa malipo wa kielektroniki, ili kuongeza udhibiti wa uwezekano wa matumizi ya hundi za kughushi.

Dkt. Kijaji alisema pamoja na kufanya mabadiliko ya Uongozi wa Shirika hilo, pia imelipatia Shirika hilo wataalam katika nyanja za mifumo ya TEHAMA na mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu (e-Office) ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji

Alisema kuwa Serikali imechukua hatua ya kuliimarisha Shirika la NIC kitaalam kwa kuliondoa shirika hilo kutoka kwenye mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa na kuliwezesha kushiriki katika biashara ya bima kwa ushindani.

Katika kuongeza udhibiti wa matumizi ya fedha za Shirika, ufungaji wa Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Kihasibu na Malipo katika Taasisi za Umma (MUSE) uko katika hatua za mwisho na kwamba mfumo huo utakapokamilika utaongeza udhibiti katika malipo yote yanayofanyika.

Alingeza kuwa Serikali inaendelea kupitia upya Mpango Mkakati wa NIC ili uendane na mahitaji halisi ya biashara ya ushindani, kuongeza uwekezaji katika mifumo ya TEHAMA ili kuwafikia wateja wengi zaidi, kuongeza ubora wa huduma na kulipa madai, kutoa gawio kubwa kwa Serikali na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya Taifa.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527