MBARAWA AMTUMBUA AFISA KITENGO CHA MANUNUZI TANGA UWASA



 WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani Tanga iliyoanza leo kushoto ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly
 Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly akizungumza wakati wa ziara hiyo kushoto ni Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo

  WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa kulia akinawa mikono kabla ya kuingia kwenye ukumbi wa mamlaka ya maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga(Tanga Uwasa) wakati wa ziara yake
  WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa kushoto akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hillywakati wa ziara yake mara baada ya kutembelea chanzo cha maji eneo la  Horohoro wilayani Mkinga katikati ni Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo
WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa kulia akiwa na
Mkurugenzi Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly wakati akitoka kutembelea miradi wa maji eneo la Horohoro

 WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa akitoka kutembelea miradi wa maji eneo la Horohoro
WAZIRI wa Maji,Profesa Makame Mbarawa amemuondoa kwenye nafasi yake aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Menejimenti ya  Manunuzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira jijini Tanga(Tanga UWASA)Jamal Ngereja kwa kushindwa kufanya taratibu za manunuzi ya mabomba na vifaa katika miradi saba ya maji katika wilaya nne mkoani Tanga inayotekelezwa na Mamlaka hiyo.


Pia Profesa Mbarawa amefanya maamuzi hayo katika Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira za Moshi,Babati na Arusha nakuahidi kuendelea kufanya  mabadiliko katika mamlaka nyingine za maji za Morogoro,Mwanza,
Tabora,Shinyanga na Kahama.


Profesa Mbarawa amefikia uamuzi huo baada ya Wizara ya Maji kutoa fedha takribani Sh.Milioni 700 katika miradi saba ya maji katika wilaya za Pangani,Mkinga,Muheza na Handeni kwa ajili ya ununuzi wa mabomba tangu mwezi Novemba mwaka jana lakini hakuna chochote kilichofanyika.


Pamoja na kufanya maamuzi hayo lakini pia aliwaonya  wahasibu katika mamlaka za maji nchini nao wajiandae iwapo tu watafanya  uzembe katika matumizi ya fedha za miradi ya maji .“Haiwezekani tumetoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maji katika mikoa ya Mbeya,Iringa na Tanga kiasi hicho hicho cha fedha lakini wenzenu wamefikia asilimia 70 ya utekelezaji  lakini Tanga hakuna kilichofanyika,”alisema.


Aliongeza, “ kutokana na hilo nakuambia kabisa wewe(Afisa Manunuzi) nakuondoa hapa na hili nitafanya pia kwenye mamlaka  za Maji Safi na Usafi wa Mazingira za Morogoro,Mwanza,Kahama,Shinyanga na Tabora kama  nilivyofanya Babati,Moshi na Arusha,”alisema.


Aidha, kwa upande wa miradi ya maji ambayo haiendi vizuri haswa ya mabwawa,Profesa Mbarawa aliahidi kuhakikisha anapeleka wataalamu kutoka wizarani kuchunguza miradi hiyo kila kitu ilikujua kama inakwenda na thamani ya fedha zilizotumika.



“Nitahakikisha kuwa ndani ya wiki kwenye miradi ya maji ambayo haiendi vizuri tunaleta wataalamu kuja kuchunguza  kila item(kitu) kuanzia tofali,urefu wa kibanda,kina cha mabwawa kuona kama inakwenda na value for money (thamani ya fedha),kutokana tumegundua kuna watu kuanzia ngazi ya Halmashauri  hadi Wizarani walihusika na hujuma za miradi ya maji kwa kupandisha gharama,”alisema.

 Aliongeza, “Nataka nimiambie wakandarasi na watumishi wa Wizara  ambao wamehusika na huo mchezo mchafu wajiandae safari hii hatuna mchezo”.


Katika hatua nyingine,Waziri Mbarawa amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/21,Serikali kupitia Wizara ya Maji imetenga fedha kwa ajili ya kutoa maji katika chanzo cha mto Zigi hadi katika mjiwa Horohoro wilayani Mkinga wenye urefu wa kilometa 40.


Amesema kuwa,mradi huo utavinufaisha vijiji zaidi ya 30 vitakavyopitiwa na mradi huo na kuahidi pia kuleta wataalamu wa Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi(DDCA) kuja kuchunguza na kufanya tathminikatika bwawa la maji la Horohoro.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527