RC TABORA ASIMAMISHA LIKIZO ZA WAGANGA NA WAUUGUZI ILI KUTOA ELIMU YA KUPAMBANA NA CORONA


MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amesimamisha kwa muda likizo za watumishi wakiwemo wa Idara za Afya ili waendelee kuunganisha nguvu katika kusaidia jamii kwenye kampeni za mapambano ya ugonjwa wa Covid -19.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwakuwepo na wataalamu wa kutosha katika maeneo yote ambao wataendelea kutoa elimu ya kujikinga na kudhibiti ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi aina ya Corona usiingie Mkoani Tabora.

Mwanri alitoa kauli hiyo  wilayani Uyui na Nzega wakati ziara yake ya kukagua Vituo na Zahanati zilizoandaliwa kwa ajili ya washukiwa wa ugonjwa wa covid -19 kama itatokea bahati wakaonekana wakaonekana Mkoani humo.

Alisema kipaumbele hivi sasa ni kuhakikisha tahadhari zote zinachukuliwa ili wakazi wa Mkoa wa Tabora waendelee kuwa salama kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu na viongozi wa Kitaifa.

Aidha Mwanri alizitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Tabora kutumia redio zilizopo na magari ya matangazo kupeleka elimu katika maeneo mbalimbali ya wananchi juu ya kujikinga na kulinda dhidi ya Covid -19.

“Tumieni magari yenye vipaza sauti kupitia katika mitaa mbalimbali kutoa elimu ya kujikinga wakati wote…na pia wataalamu nendeni katika Redio zote zilizopo mkoani Tabora kupeleka ujumbe ambao utawasaidia wananchi kuepuka kupata maambukizi ya Corona” alisema.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa ameziagiza Halmashauri zote kuhakikisha magari yote ya abiria yanayosafirisha abiria ndani na nje Mkoa wa Tabora yanapuliziwa dawa kabla ya safari ili kuwakinga abiria ya uwezekano wa kupata corona.

Alisema ni lazima gari linapofika Stendi lipuliziwe dawa na taarifa zake zijazwe kwenye fomu ili kuonyesha kuwa limetekeleza agizo hilo ndio liruhusiwe kupakia abiria na kuendelea na safari zake.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post