RAIS WA URUSI VLADIMIR PUTIN 'AJIFUNGIA NYUMBANI' KUKABILIANA NA CORONA


Rais wa Urusi Vladimir Putin kuanzia sasa atakuwa akifanya kazi akiwa nyumbani kwake huko Novo-Ogarevo, karibu na jiji la Moscow, msemaji wa Kremlin amesema siku moja baada ya daktari aliyekutana na rais Putin wiki iliyopita kupatikana na virusi vya Corona.

Kiongozi wa Urusi anatarajiwa leo mchana kuongoza mkutano na wajumbe wa serikali yake kwa njia ya video, Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari, akibaini kwamba Vladimir Putin, ambaye kwa mujibu wa Kremlin yuko katika afya njema, sasa ameamuwa kutumika akiwa nyumbani kwake.

"Kila mtu sasa anajitenga na wengine kutokana na hali inayojiri kwa sasa," Dmitry Peskov ameongeza.

Visa 2,777 vya maambukizi ya virusi vya Corona vimethibitishwa nchini Urusi ambapo watu 24 wamefariki dunia kwa ugonjwa huo ambao ulianzia nchini china mwezi Desemba mwaka 2019, kabla ya kusambaa katika zaidi ya nchi 200 kote ulimwenguni.

Katika kujaribu kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona, hasa katika mji mkuu, ambao umekuwa kitovu cha janga nchini, siku ya Jumapili manispaa ya mji wa Moscow ilitangaza marufuku ya kutoka nje.

-RFI


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527