WAKAMATWA NA POLISI KWA KUSAMBAZA MTANDAONI VIDEO YA MTOTO WA MIAKA 3 WAKIMNYWESHA BIA BAA


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba 

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu watatu kwa kosa la kumpeleka Baa mtoto  wa kike mwenye umri wa miaka mitatu na kumnywesha pombe aina ya Balimi huku wakimrekodi video kisha kusambaza kwenye mitandao ya Kijamii yakiwemo magroup ya Whatsapp.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea Aprili 24,2020 majira ya saa sita mchana kwenye baa iitwayo Bondeni iliyopo katika Kijiji cha Nyaligongo, Kata ya Mwakitolyo, Wilayani Shinyanga. 

“Tunawashikilia watu watatu ambao ni Godius Novat Katisha (32),mkazi wa Mwakitolyo ambaye ni baba wa mtoto huyo, mmiliki wa bondeni bar aitwaye Irene Alphonce Pima (32), mkazi wa Namba 02 Mwakitolyo na Oscar Daniel Makondo (35) mkazi wa mtaa wa Mayila Kahama kwa Makosa ya Ukatili dhidi ya Mtoto na Matumizi Mabaya ya Mitandao”,amesema Kamanda Magiligimba. 

“Siku ya tukio Mtoto wa kike, mwenye umri wa miaka mitatu, mkazi wa Mwakitolyo alifanyiwa ukatili kwa kupelekwa kwenye baa hiyo na kunyweshwa pombe aina ya Balimi na kurekodiwa video kwa kutumia simu kisha kurushwa kwenye mitandao ya kijamii na kuonekana kwenye magroup ya whatsapp”,ameeleza Kamanda Magiligimba. 

Amesema baada ya tukio hilo kikosi Kazi cha askari wa Uhalifu wa Makosa ya Kimtandao waliwakamata watuhumiwa hao akiwemo baba mzazi wa mtoto aitwaye Godius Novat Katisha. 

Kamanda Magilgimba amesema watuhumiwa watafikishwa Mahakamani baada ya upelelezi kukamilika huku akitoa wito kwa wananchi kuheshimu haki za mtoto na yeyote atakayeenda kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Katika Video hiyo iliyosambaa mtandaoni ambayo Malunde 1 blog pia imefanikiwa kuiona inamuonesha mtoto huyo akiwa anakunywa pombe aina ya Balimi huku akikohoa baadhi ya watu wanasikika wakicheka pamoja na sauti ya mwanaume akimhamasisha mtoto anywe pombe akimaliza amnunulie nyingine.

"Yaani hii ni Live ..unasikia Nkurunzinza..halafu Nkurunzinza usicheke sana Nkurunzinza..Kunywa kunywa nyingine nikununulie", sehemu ya maneno yanayosikika katika video hiyo ambayo imeibua hisia tofauti kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post