NIDA YAWATAKA WANANCHI KUEPUKA VISHOKA WAKATI WA MCHAKATO WA KUOMBA VITAMBULISHO VYA TAIFA

Na: Hadija Maloya-NIDA.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewaasa wananchi kuacha kutumia njia na watu wasio rasmi kisheria maarufu kama vishoka wakati wa mchakato wa kuomba Vitambulisho vya Taifa badala yake wafuate utaratibu rasmi uliowekwa na Serikali katika kuomba Vitambulisho hivyo.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Bw. Geofrey Tengeneza kufuatia tukio la mwananchi mmoja (Jina limehifadhiwa) mkazi wa Kigogo fresh jijini Dar es salaam kufika ofisi ya NIDA Wilaya ya Ilala iliyoko Ukonga Mombasa kupiga picha ya Kibaometriki kwa ajili ya Kitambulisho cha Taifa, kuwadokeza Maafisa usajili wa NIDA kuwa mara baada ya kukamilisha zoezi hilo la kupiga picha ameelekezwa na mtu mmoja kupeleka fomu yake ya maombi kwake ili amkamilishie vipengele vilivyobaki pamoja na kumpatia cheti cha kuzaliwa.

Mwananchi huyo alisema kuwa hata fomu yake ya maombi ya Kitambulisho cha Taifa imesainiwa na kugongwa muhuri na mtu huyo na kumpata barua baada ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa anakoishi wa Kigogo Fresh kukataa kutoa barua na kusaini fomu zake kutokana na kutokuwepo kwa cheti cha kuzaliwa kama utaratibu unavyotaka.

Mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni na kisha kufanyiwa upekeuzi kwenye ofisi yake katika duka moja la steshenari lililoko Ukonga Mombasa ambako walikuta nyaraka mbalimbali za Serikali kama vile nakala za Fomu za Maombi ya Vitambulisho vya Taifa (F1A) ambazo tayari zimegongwa muhuri, nakala za Hati za Kiapo cha Kuzaliwa (Affidavit form) na nakala za barua za Utambulisho wa Makazi zenye muhuri wa ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mwembe Madafu.

Mtuhumiwa huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, tayari amefunguliwa mashtaka kwa kosa la kukutwa na Nyaraka za Serikali kinyume cha sheria na kosa la kujifanya Afisa wa NIDA.

Akizungumzia tukio hilo Bw. Tengeneza amesema mtu huyo atakuwa ni kishoka ambaye bila shaka hata muhuri wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa aliogonga na barua ya Serikali ya Mtaa aliyoitoa kwa mwananchi huyo ili awasilishe katika ofisi ya NIDA wilaya ya Ilala kwa ajili ya kupatiwa Kitambulisho cha Taifa, vitakuwa vyote ni feki. 

Ameonya watu wanaojihusisha na kuwarubuni wananchi waache tabia hiyo mara moja kwani Mamlaka haitasita kuwachukulia hatua kali za sheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha Mahakamani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post