MKANDARASI AZUIWA KUTOKA NJE YA MKOA WA SONGWE


Mkandarasi wa Mradi wa maji wa Iyula uliopo Wilaya ya Mbozi amezuiwa kutoka Nje ya Mkoa wa Songwe huku akiwekwa chini ya uangalizi wa jeshi la Polisi mpaka atakapo kamilisha vifaa na wataalamu watakaomalizia Mradi huo.


Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ametoa zuio hilo leo mara baada ya kutembelea Mradi wa maji wa Iyula ambao ulitarajiwa kukamilika tangu mwaka 2017 huku ukiwa na thamani ya shilingi bilioni tano.

Brig. Jen. Mwangela amesema mkandarasi huyo anatakiwa aweke vifaa vyote na wataalamu wote watakao muwezesha kukamilisha ujenzi wa mradi huo ndipo ataruhusiwa kutoka nje ya Mkoa wa Songwe.

Ameongeza kuwa mkandarasi huyo aliweka masharti ya kupewa fedha nyingi ambapo tayari ameshapewa sehemu ya fedha hizo lakini bado utendaji wake wa kazi umekuwa wa kusuasua huku wananchi wakiendelea kupata adha ya kukosa maji.

Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Songwe Mhandisi Charles Pambe amesema mradi wa Maji wa Iyula una gharimu shilingi bilioni tano na tayari Mkandarasi ameshapewa bilioni 2.2

Mhandisi Pambe amesema kutokana na kusuasua kwa mkandarasi huyo RUWASA wana angalia uwezekano wa kuujenga mradi huo wenyewe kwa kutumia Force Account.

Naye Mkandarasi wa Mradi wa maji wa Iyula kutoka STC Construction ya Dar es Salaam Alan Makame amesema kusuasua kwa mradi huo ni kutokana na kucheleweshewa malipo pamoja na RUWASA kutotembelea mradi huo.

Amesema ndani ya siku tatu atakuwa ameanza kazi ya kuweka baadhi ya mabomba katika mradi huo na kuwa baada ya wiki mbili atakuwa amekamilisha mradi huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527