KANISA KATOLIKI KAGERA LASITISHA IBADA NA SALA ZA JUMUIYA ILI KUKABILIANA NA KUSAMBAA KWA CORONA


Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki la Rulenge- Ngara mkoani Kagera, limesitisha ibada za misa, maadhimisho mengine yanayokusanya waumini wengi kanisani na sala za jumuiya kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Jumapili Aprili 19.


Katika taarifa yake Askofu wa jimbo hilo, Severine Niwemugizi amesema baada ya muda uliopangwa kumalizika wataangalia hali itakavyokuwa na ikibidi muda wa kusitisha ibada utaongezwa.

“Baada ya kutafakari alama za nyakati na kujifunza kutoka kwa wenzetu Ulaya na Marekani, nchi jirani zetu na hatua ambazo Baba Mtakatifu alizichukua kwa kutoa maelekezo kwa Maaskofu Wakatoliki duniani namna ya kuadhimisha ibada katika kipindi hiki cha vita dhidi ya corona, nimebeba dhamana ya kutoa uamuzi mgumu.

“Tutaomba redio Kwizera irushe adhimisho la misa fupi ili waumini wafuatilie redioni na baada ya muda huo kumalizika tutaona hali itakuaje na ikibidi tuongeze muda tutafanya hivyo,” amesema Askofu Niwemugizi.

Aidha amewataka mapadre kuadhimisha misa peke yao kwa niaba ya waumini kuwaombea na kuiombea dunia ili Mungu atunusuru na janga hili na kuagiza sala za Jumuiya kufanyika ndani ya familia kwa familia moja moja.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527