JESHI LA POLISI KITENGO CHA USALAMA BARABARANI MKOA WA SHINYANGA LATOA ELIMU YA KUJIKINGA NA COVID 19


Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani mkoani humo, Africanus Sulle 

Salvatory Ntandu - Shinyanga
Katika jitihada za kuhakikisha abiria wanakuwa salama na wanajinga na Ugonjwa hatari wa homa ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona katika vyombo vya Usafiri Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama barabarani mkoa wa  Shinyanga limeanza kutoa elimu kwa watumiaji wa vyombo vya Moto sambamba na kukagua utekelezaji wa maelekezo serikali kuhusiana na  COVID 19.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi leo Aprili 22,2020 mwaka  huu Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani mkoani humo, Africanus Sulle alisema kuwa Elimu hiyo imeanza kutolewa tangu Aprili 16 na inatolewa katika vituo vyote vya mabasi  mkoani Shinyanga vinafanyiwa ukaguzi wa kina  kuhusiana namna ya kujikinga na Ugonjwa wa COVID 19.

Alisema kuwa kwa sasa wanahakikisha Mabasi ya abiria hayazidishi abiria sambamba na kuviondoa viti ambavyo wamiliki wa mabasi wameviweka ambavyo vinasababisha abiria kusongamana kinyume na maelekezo ya serikali.

“Tumejipanga kikamilifu Askari wetu wapo katika vituo vyote vya Mabasi mkoani humu, kuhakikisha wanakagua magari yote yanayoingia na kutoka ili kuhakikisha kama wanandoo za maji pamoja na vitakasa mikono (sanitizer)ili kuhakikisha kabla ya kuanza safari ni lazima wanae na wapofika pia ni muhimu kunawa mikono ili kujiweka salama”,alisema Sulle.

Pia Sulle alifafanua kuwa serikali imeagiza kuviondoa viti vilivyowekwa kwenya mabasi madogo aina ya Hice ili kupunguza msongamano kwa jambo ambalo limekuwa likisababisha abiria  kusogeleana na kila mmiliki wa gari anapaswa kuhakikisha anatekeleza agizo hilo.

“Tangu tumeanza ukaguzi Aprili 17 mwaka huu mwitikio umekuwa mzuri na tunaimani elimu tuliyowapatia abiria na wamiliki wa magari imeleta matokeo chanya kwani kila mmoja ameanza kutimiza wajibu wake pindi anapokwa anataka kusafiri kwa kuchukua tahadhari ya Ugonjwa wa COVID 19.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kituo cha Mabasi cha CDT ,Kahama Sylivesta Joseph alisema  baada ya serikali kutoa maelekezo hayo utekelezaji ulianza mara mmoja ambapo kwa sasa katika kituo hicho abiria haruhusiwi kuingia bila kuna mikono.

“Abiria wanaokaidi kunawa mikono wanakamatwa na migambo ambao tumewaweka na wanapelekewa kituo kidogo cha polisi CDT na hutozwa faini ambapo mpaka sasa zaidi ya abiria 6 walishakamtwa na kutozwa faini na idara ya afya ya Halmashauri ya Mji kwa kutotii maagizo ya serikali”,alisema Joseph.

Nae Masanja Duttu mmoja wa abiria alisema serikali inapaswa kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote wanaokaidi kunawa mikono kwa maji na sabuni wanaoingia katika kituo hicho.

“Haiwezekani suala hili liendelee kufanyiwa mchezo chukueni hatua kali kwa watu wote bila upendeleo kwani asili ya watu wa kanda hii ya ziwa hawapendi kunawanawa kila mara jambo ambalo kwao linawawia ugumu kwani hawajazoea,”alisema Duttu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527