WANNE WADAKWA NA DAWA ZA KULEVYA NYUMBANI KWA CHIKU SHINYANGA MJINI


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia wanaume watatu na mwanamke mmoja kwa tuhuma ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroine katika mtaa wa Majengo, Kata ya Kambarage  Manispaa ya Shinyanga. 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema watu hao wamekamatwa Aprili 19,2020 baada ya askari polisi kupata taarifa za kiintelejensia. 

“Askari walifika nyumbani kwa mtuhumiwa Chiku Tungu na kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa ndani ya uzio wa nyumba hiyo na dawa hizo ambazo ni pinchi 08 za heroine pamoja na rizla, kitezo, kigae na kisu kimoja”,amesema Kamanda Magiligimba. 

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Hassan Ibrahim (22), mkazi wa Majengo, Juma Omary (26), mkazi wa Ngokolo, Abdalah Hemed (23), mkazi wa Majengo pamoja na mwanamke mmoja aitwaye Chiku Tungu (57), mkazi wa Majengo. 

“Watuhumiwa wanahojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani. Natoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutokomeza uuzwaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya ili kuikinga jamii dhidi ya dawa hizo”,amesema Kamanda Magiligimba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post