ALIYEPIGA SIMU KWA WAZIRI WA AFYA AKIDANGANYA ANA UGONJWA WA CORONA AKAMATWA SHINYANGA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba 
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia Mussa Jackson Kisinza, (25) mkazi wa kijiji cha Mwakitolyo namba 02 wilaya ya Shinyanga kwa  kutoa taarifa ya uongo kwa kumpigia simu na kumdanganya Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kuwa ana ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba baada ya kijana huyo kutoa taarifa kuwa ana ugonjwa wa Corona timu ya madaktari inayotoa huduma eneo la halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (vijijini) kuhusiana na ugonjwa wa Covid 19 ilifika eneo la kijiji cha Mwakitolyo namba 02 ili kutoa huduma kwa mtu huyo lakini mtu huyo alizima simu yake na kusababisha timu hiyo ya madaktari kushindwa kumpata hivyo kusababisha taharuki. 

“Hivyo Aprili 15,2020 majira ya saa moja kamili asubuhi kikosi kazi cha askari wa makosa ya kimtandao walifika eneo la Mwakitolyo namba 02 na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo Mussa Jackson akiwa anaendelea na shughuli zake za machimbo na kumfikisha zahanati ya kijiji cha mwakitolyo namba 02”,ameeleza Kamanda Magiligimba. 

“Timu ya madaktari ilimfanyia vipimo vya awali vya magonjwa nyemelezi yanayoashiria kuwepo kwa uwezekano wa mtu kuwa na ugonjwa wa Covid 19 lakini hakuwa na dalili za magonjwa hayo”,ameongeza Kamanda Magiligimba. 

Amesema baada ya kuhojiwa mtuhumiwa amekiri kutoa taarifa hiyo na kwamba baadaye aliamua kuiharibu laini yake ya simu kwa kuivunja vunja. 

“Natoa wito kwa wananchi kuacha masihara juu ya ugonjwa Covid 19 na mtu yeyote atakayetoa taarifa za uongo juu ugonjwa huo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake”,amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post