WIZARA YA AFYA YATANGAZA NAFASI 1000 ZA MADAKTARI


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetangaza nafasi mpya elfu moja za ajira kwa kada ya madaktari daraja la pili.

Tangazo hilo la nafasi za ajira limetolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt Zainab Chaula, ambapo kati ya nafasi hizo madaktari 610 watakwenda kufanya kazi katika hospitali za wilaya zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Madaktari 306 ni kwa ajili ya hospitali za mikoa na zile za Rufaa, arobaini watapelekwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam na wengine Ishirini katika hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma.

Katika mgawanyo wa nafasi hizo mpya za madaktari, Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) itapata madaktari kumi, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete madaktari saba na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road nayo pia madaktari saba.

Februari Ishirini mwaka huu wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya madaktari kitaifa kwa mwaka huu, Rais John Magufuli aliahidi kutangaza nafasi za ajira mpya elfu moja za madaktari, madaktari ambao baada ya kuajiriwa watapangiwa kufanya kazi kwenye maeneo yenye upungufu.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527