Waziri Wa Mambo Ya Nje Prof. Kabudi Awasilisha Ujumbe Maalum Wa Rais Magufuli Kwa Rais Donald Trump Wa Marekani

Washington,Marekani,
Tanzania na Benki ya Dunia zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu,uendelezaji wa miundo mbinu na masuala ya kijamii kupitia mikopo,ruzuku na misaada inayotolewa na benki hiyo ili kuisaidia Tanzania kupiga hatua za kimaendeleo na kutokomeza umasikini miongoni mwa raia wake.

Hayo yamebainika baada ya mazungumzo baina ya Mkurugenzi mtendaji wa benki ya Dunia anayeiwakilisha Marekani Dkt. Jennifer "DJ" Nordquist na Mjumbe maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi mazungumzo yaliyofanyika katika makao makuu ya Benki hiyo Washington Marekani ambapo wamejadili masuala mbalimbali hususani kuhusu masuala ya mahusiano baina ya Benki ya dunia,Marekani na Tanzania.

Pia wamezungumzia masuala mbalimbali ya miradi maendeleo ikiwa pamoja na sekta ya elimu na kujadili maeneo mbalimbali ambayo Benki hiyo imeisaidia Tanzania aidha kwa mikopo ya masharti nafuu au misaada ikiwa ni pamoja na ujenzi na uendelezaji wa shule za msingi na sekondari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeiwakilisha Marekani Dkt. Jennifer "DJ" Nordquist  amesema anafuatilia kwa ukaribu masuala yote yanayoendelea Tanzania na kwamba anavutiwa na mambo ya maendeleo yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli katika utoaji wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.

Aidha Dkt Jennifer "DJ" Nordquist ameeleza kufurahishwa kwake na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali na kusisitiza kuwa ni vyema elimu inayotolewa isiwe na ubaguzi na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kuoata fedha ziatakazowezesha kuboresha miundombinu ya elimu nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabweni katika shule za kata na kutoa mfumo maalum wa utoaji wa elimu kwa wanafunzi wanaokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wale wanaopata ujauzito.

Mkurugenzi Mtendaji mbadala wa Kanda Namba 1 ya Afrika kutoka Benki ya Dunia Bw. Taufila Nyamadzabo amesema mazungumzo baina ya Tanzaia na benki ya dunia yamekuwa ni ya manufaa kwa kuwa yameondoa sintofahamu iliyokuwepo kati ya pande hizo mbili na ni matumaini yake mradi huo utapitishwa na bodi ya benki ya dunia hivi karibuni.

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharki Prof. Palamagamba John Kabudi amewasilisha ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kweda kwa Rais wa Marekani Mhe. Donald Trump kupitia Wizara ya mambo ya Nje ya Marekani.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye pia anashughulikia masuala ya Afrika Mhe. Tibor Nagy ndiye aliyepokea ujumbe huo na kuahidi kuendeleza mashirikiano mazuri naya muda mrefu yaliyopo kati ya Tanzania na Marekani. Katika mazungumzo hayo Naibu Waziri huyo ameambatana  na Balozi Mteule wa Marekani Nchini Tanzania Dkt. Donald Wright


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post