BENKI YA CRDB YAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI 2020 KWA KUHAMASISHA USAWA WA KIJINSIA KATIKA JAMII

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akifungua sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa wafanyakazi wa Benki ya CRDB

Benki ya CRDB imefanya hafla ya kusherehekea ‘Siku ya Wanawake Dunia’ ikilenga kuhamasisha usawa wa kijinsia katika jamii. Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema Benki ya CRDB inachukulia kwa umuhimu suala la kumuwezesha mwanamke na ndiomana Benki hiyo imetoa kipaumbele cha ajira kwa wanawake katika ngazi mbalimbali. “Asilimia 46 ya wafanyakazi wetu ni wanawake, na tunatamani kuona tunaongeza kufikia asilimia 50,” alisema Nsekela.

Nsekela alisema Benki ya CRDB pia inafanya jitihada za kuwanyanyua wanawake kupitia nafasi za uongozi huku akibainisha kuwa Benki hiyo ina jumla ya wanawake viongozi 284 katika ngazi za umeneja, wakuu wa vitengo na wakurugenzi. Nsekela alisema Benki ya CRDB imedhamiria kujenga mazingira, rahisishi, mazuri na rafiki ya kujenga usawa ili kuwasidia wanawake waweze kukua katika mazingira yao ya kazi.

Katika hafla hiyo Benki ya CRDB pia ilizindua kampeni maalum ya kusaidia kutoa taulo za kike (sanitary pads) kwa wanafunzi mashuleni. Kampeni hiyo ilianza kwa kuzindua zoezi la uchangiaji lilokuwa likiendeshwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa ambapo wafanyakazi wa Benki ya CRDB wamejitokeza kuchangia gharama za ununuzi wa taulo hizo. 

“Tunashukuru Mkurugenzi wetu Mtendaji ametufungulia kwa kuchangia kiasi cha shilingi milioni 1, hii ni zawadi ya kipekee kwa wanawake wote lakini pia inaonyesha ni kwa namna gani anawathamini wake,” alisema Mwambapa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Mwambapa akiendesha zoezi la uchangiaji kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa taulo za kike (sanitary pads) kwa wanafunzi mashuleni.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Mwambapa na viongozi wengine wanawake wakishangilia baada ya Mkurugenzi Mtendaji, Abdulmajid Nsekela kuchangia shilingi milioni moja kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wakike

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Benki ya CRDB, Siophoro Kishimbo alisema Benki hiyo imeweka mikakati endelevu ya kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanawake wa Benki hiyo wanapata fursa sawa na wanaume. 
“Tunaihamasisha jamii kuzingatia usawa katika sehemu zote iwe ni kwenye kazi na hata nyumbani kwenye familia hii itaongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo na hivyo kujenga taifa imara zaidi,” alisema Kishimbo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post