WAZIRI MKUU MAJALIWA APIGA MARUFUKU UCHIMBAJI WA MADINI LUSHOTO

 WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Magamba Kata ya Magamba wilayani Lushoto wakati wa ziara yake
 WAZIRI wa Madini Dotto Biteko akizungumza wakati wa ziara hiyo
MKUU wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella akizungumza wakati wa ziara hiyo


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesitisha zoezi la uchimbaji wa madini ya Boxite katika mgodi uliopo Kata ya Magamba wilayani Lushoto.

Pia,amemuagiza Waziri wa Madini Dotto Biteko kuzichukua leseni zote 22 za wachimbaji wakubwa na wadogo zilizotolewa katika mgodi huo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo wakati alipoutembelea mgodi huo katika ziara yake wilayani Lushoto.

Amesema kuwa,serikali ilipokea malalamiko ya wananchi kuhusu athari uchimbaji madini katika mgodi huo zikiwemo uharibifu wa mazingira na athari za kiafya.

Pia amesema kutokana na uzito wa mgogoro uliobuka katika mgodi huo,Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa alimuagiza kufuatilia wakati wakiwa Msumbiji kwenye hafla ya kuapishwa Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi kuwa atembelee wilayani Lushoto kusikiliza kilio cha wananchi na atoe tamko la serikali. 

Amesema kuwa serikali imefanya maamuzi hayo kutokana inasikiliza wananchi wake kutoka na hoja zao walizozitoa.

" Serikali imefanya maamuzi,imesitisha kila kitu baada ya kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu kero na athari za afya zinazotokana na uchimbaji huo,"alisema.

Aliongeza, "Waziri wa Madini chukua  leseni zote 22 za uchimbaji madini zilizotolewa eneo hilo na wananchi lindeni eneo hilo wasiingie watu kuchimba,"alisema.

Kwa upande wake,Waziri Biteko alisema kuwa mgogoro huo wa kuzuia uchimbaji katika mgodi huo ulianza muda mrefu lakini mwezi August 30,mwaka jana walifanya mkutano mkubwa na wananchi na kutoa malalamiko mengi ikiwemo athari zinazotokana na uchimbaji huo.

Alifafanua kuwa baada ya kusikiliza maoni hayo,September 4,mwaka jana waliandika barua wa wachimbaji wote kusitisha zoezi la uchimbaji katika mgodi huo.

Mbunge wa jimbo la Lushoto Shabani Shekilindi alisema kuwa eneo hilo ndio chanzo kikubwa cha maji katika maeneo mbalimbali katika jimbo hilo,hivyo uchimbaji huo una athari kubwa za kiafya na kimazingira.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post