WAZIRI MKUU ASEMA SERIKALI IMEZUIA UINGIZWAJI WA SARUJI KUTOKA NJE YA NCHI ILI KULINDA VIWANDA VYA NDANI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wawekezaji katika sekta mbalimbali nchini wakiwemo wenye viwanda vya kuzalisha saruji.

Amesema katika kuhakikisha inalinda viwanda vya ndani vya kuzalisha saruji Serikali imeamua kuzuia uingizwaji wa saruji kutoka nje ya nchi.

Waziri Mkuu aliyasema hayo leo(Jumanne, Machi 3, 2020) wakati akizungumza na watumishi wa kiwanda cha saruji cha Simba alipotembelea kiwanda hicho akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga.

Amesema licha ya Serikali kupata kodi kutokana na uwepo wa kiwanda hicho, pia kimesaidia katika kutatua changamoto ya ajira hususani kwa vijana.

Naye, Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuwa wanazingatia sheria zote za madini ukilinganisha na viwanda vingine.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Reinhardt Swart alisema kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha tani milioni 1.25 kwa mwaka lakini kutokana na mahitaji ya soko kinazalisha tani milioni 1.075 kwa mwaka.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kiwanda hicho kimeajiri jumla ya wafanyakazi 319 kati yao wazawa ni 316 na watumishi watatu ni raia ya kigeni.

Pia, Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post