MATATANI KWA TUHUMA YA KUJIUNGANISHIA MAJI YA KUWASA KWA NJIA ISIYO HALALI KAHAMA MJINI

NA SALVATORY NTANDU - KAHAMA

Mkazi wa mtaa wa Lugela Kata ya Nyahanga wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Ismail Kitinga anashikiliwa na jeshi la Polisi wilayani humo kwa mahojiano baada ya kutuhumiwa kujiunganishia maji kwa njia isiyo halali kutoka Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa mazingira Mjini Kahama (KUWASA).

Akizungumza na waandishi wa katika eneo la Tukio  Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini kahama(KUWASA) Misana Shija alisema kuwa Ismail alijiunganishia huduma ya Maji kinyume na utaratibu na Mamlaka hiyo kuisababisha hasara serikali.

“Ismail ni mteja wa KUWASA  tumebaini kuwepo uchepushaji wa maji kabla ya kufika kwenye mita yetu ambayo tumemwekea huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kuikosesha mamlaka ya mapato,”alisema Shija.

Misana alifafanua kuwa baada ya matumizi ya maji kushuka ya Ismail kutoka uniti 20 kwa mwezi hadi Uniti moja ndipo mafundi wa mamlaka walipofika  nyumbani kwake kufuatilia mfumo wa maji na kubaini kuwepo kwa maunganisho yasiyo halali.

“KUWASA inaendelea na zoezi la kubaini wateja wake ambao wanatumia maji nje ya mfumo na kuwataka wateja wote wanaojiuhisha na vitendo  hivyo kuacha mara moja kwani watakao bainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ”alisema Misana.

Kwa upande wake Ismail Kitinga ambaye anatuhumiwa kuhujumu miundombinu ya maji amekiri kutokea kwa wizi wa maji katika nyumba yake na kusema  kuwa yeye hakuwa na taarifa za kuwepo kwa wizi huo kwani hapo awali alishatoa taarifa za kuibiwa mita katika Idara ya Maji, na kuomba kuwekewa mita nyingine ambayo iliwekwa ndani ya uzio wa nyumba yake.

“Mimi binafsi sijui aliyefanya maunganisho haya ila mimi ninachojua ni kwamba walikuja mafundi kutoka KUWASA na kuniwekea mita mpya hapa kwangu baada ya zamani kuibiwa na watu wasiojulikana,siwezi kuiba maji kwani ninauwezo wa kulipa maji”alisema Kitima.

KUWASA inaendelea na zoezi la kukagua miundombinu ya maji kwa wateja wake ili kubaini wanaotumia maji nje ya mfumo ambao unaisababishia hasara Mamlaka na serikali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post