AHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA KWA KUUA NA KISHA KUPORA MILIONI 1, CHUPA YA CHAI NA SIMU


Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, imemuhukumu kunyongwa hadi kufa mkazi wa Kijiji cha Kibubwa, Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Waryoba Elias baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki kumuua Chacha Ibuga usiku wa kuamkia Novemba mosi, 2017.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, John Kayohoza, alimkumbushia mshtakiwa shtaka lililokuwa linamkabili katika kesi hiyo namba 33/2019.

Jaji Kayohoza akisoma mazingira ya kesi na ushahidi wa mashahidi watano, ilielezwa Novemba mosi, 2017 saa 6.00 usiku, mshtakiwa akiwa na wenzake watano ambao hawajafahamika, wakiwa na tochi mbili na mapanga, walivamia nyumbani kwa Chacha Isoye Ibuga.

Ilielezwa wakati Ibuga akiwa ndani, kabla ya kuvamiwa alisikia mbwa wake anabweka na kuamua kutoka nje kuona kuna nini na ghafla watu hao walimshambulia kwa kumkatakata sehemu mbalimbali za mwili, hasa kichwani na kupiga kelele kuomba msaada, ndipo mke wake, Lucy Lukondo alilazimika kutoka kwa lengo la kumsaidia.

Wakati Lucy anatoka ndani, alikutana na watu watatu na kumzuia na kumlazimisha kuingia ndani kumtaka awape fedha.

Kwamba mshtakiwa huyo kwa kushirikana na wenzake walifanya upekuzi ndani ya chumba alichokuwa analala marehemu na mke wake na kufanikiwa kupora fedha taslimu Sh milioni moja, chupa moja ya chai na simu moja ya mkononi.

Imeelezwa miongoni mwa watu walioingia ndani, aliyekuwa mmoja wa washtakiwa alikuwa ni jirani yao ambaye anamwita marehemu mjomba.

Watu hao baada ya kutekeleza ukatili huo, walitoweka na kwenda kusikojulikana huku majeruhi Ibuga akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Butiama ambako baadaye alifariki dunia na baada ya siku kadhaa mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani.

-Mtanzania


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post