VIJIJI 8,641 VYAFIKIWA NA UMEME WA REA

Na Mwandishi Wetu

Jumla ya vijiji 8,641 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa  na umeme kupitia Mradi ya Usambazaji Umeme Vijijini (REA) sawa na asilimia 70.4.

Hayo yamesemwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango wakati akitoa Tathmini ya Utekelezaji wa Mpango wa mwaka 2019/20 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/21.

“Katika kipindi cha Julai 2015 hadi Januari 2020, jumla ya shilingi trilioni 1.53 zimetumika katika utekelezaji wa mradi huu ikijumuisha shilingi bilioni 207.2 zilizotolewa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020.” Alisema Dkt. Mpango.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mpango alisema kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani imeendelea kuwa tulivu kwa kipindi chote cha mwaka 2019.

Ameeleza kuwa utulivu wa sarafu ya Tanzania dhidi ya sarafu kubwa duniani umetokana na utekelezaji mzuri wa sera ya fedha na ya kibajeti, pamoja na kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje.

Kwa upande wa afya, Waziri Mpango ameeleza kuwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kugharamia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vituo 540 vituo vya afya 361, hospitali za halmashauri za wilaya 71, hospitali za zamani tisa na zahanati 99 ambapo watumishi  477 wameajiriwa na kupangwa kwenye vituo hivyo.

Dkt. Mpango  alifafanua kuwa katika kipindi cha Julai 2015 hadi Januari 2020 jumla ya shilingi trilioni 3.01 zimetumika kugharamia huduma za afya ikijumuisha shilingi bilioni 14.5 zilizotumika kununua mashine ya Positron Emmission Tomography (PET scan) kwa ajili ya hospitali ya Ocean Road.

Akiongelea kuhusu mkakati wa uwezeshaji wa kaya maskini kiuchumi, amesema kuwa kwa sasa Serikali inatekeleza Awamu ya III ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III), ambapo jumla ya kaya 1,067,041 zenye wanakaya 5,130,001 zimetambuliwa na kuandikishwa katika vijiji na mitaa 9,627 kwenye Halmashauri 159 Tanzania Bara na kaya 32,248 zenye wanakaya 169,999 katika shehia 204 za Zanzibar na ruzuku ya fedha shilingi bilioni 968.73 imehawilishwa katika kaya hizo.

Amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 935.94 ni kwa ajili ya kuhudumia Kaya zilizopo Tanzania Bara na shilingi bilioni 32.79 ni kwa ajili ya Kaya zilizopo Zanzibar.

Aidha, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020, ufanisi wa kukusanya mapato ya kodi umeimarika na kufikia asilimia 96.9 ya lengo ikilinganishwa na ufanisi wa asilimia 88.6 katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, sawa na ukuaji wa asilimia 16.6.

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post