UPINZANI WAITAKA SERIKALI KUFUNGA MIPAKA KUJIKINGA NA CORONA


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeitaka serikali kuhakikisha inafunga mipaka yote ili kutoruhusu wageni na hata Watanzania waliopo nje ya nchi kwa lengo la kutoleta maambukizi mapya ya virusi vya corona.

Aidha, imesema wageni hao waruhusiwe pale inapobidi kuingia na serikali iwaweke kwenye karantini kwa gharama zao kwa siku 14 kama taratibu za kitabibu zinavyoelekeza.

Waziri Kivuli wa Afya, Cecilia Paresso ametoa rai hiyo jana Ijumaa Machi 20, ambapo amesema hii ni kwa sababu wagonjwa wote waliothibitika kuwa na virusi hivyo ni wale waliotoka nje ya nchi na si waliokuwa hapa nchini.

“Tunatambua athari za kufunga mipaka ya nchi katika wakati huu wa utandawazi wa kibiashara na kiuchumi. Hata hivyo, afya na uhai wa binadamu haiwezi kulinganishwa na thamani ya kitu chochote.

“Ni vema kwa sasa tusiangalie na kuwaza tu faida za muda mfupi katika za utalii, biashara na uchumi kwa kuacha mipaka wazi jambo ambalo litakuja kutufanya tujute baadaye kama Taifa.

“Hata hivyo tumeshangaa kupitia vyombo vya habari kumsikia Mkuu wa Mkoa wa Arusha akieleza umma kuwa dereva aliyemwendesha Mtanzania wa kwanza aliyegundulika na virusi vya corona kuwa hana maambukizi yoyote, jambo la kujiuliza hapa je siku 14 zimetimia? Kwani ni takribani siku nne tu zimepita tangu dereva huyo atafutwe na kupatikana,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, amesema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali na viongozi waliopo madarakani kutoleta mzaha kwenye suala hilo na pengine ikawa bora zaidi kuwaachia wasemaji wa jambo lenyewe kuweza kulitolea ufafanuzi kuliko hivi sasa hali inayoleta mkanganyiko wa matamko kutoka kwa kila mtu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post