Polisi Mkoa wa Morogoro nchini Tanzania inamshikilia Rehema Fabiani (18), mfanyakazi wa Mgahawa wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) akidaiwa kutoa mimba akiwa katika nyumba ya kulala wageni ya EM mjini Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Ijumaa Machi 20, 2020 Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alisema binti huyo alikutwa katika nyumba hiyo akiwa tayari katoa mimba na kusababisha kifo cha kichanga chenye jinsi ya kiume.
Mutafungwa alisema tukio hilo limetokea Alhamisi Machi 19, 2020 saa 3 asubuhi katika nyumba hiyo ya kulala wageni eneo la mtaa wa Amani kata ya Mjimkuu.
Alisema binti huyo alifika katika nyumba hilo na kupanga chumba namba saba na siku iliyofuata asubuhi mhudumu wa nyumba hiyo alisikia kelele kutoka ndani ya chumba hicho na kumgongea.
Kamanda huyo anasema baada ya kufungua mlango wa chumba na kuingia ndani alimkuta binti huyo akilalamika maumivu makali ya tumbo na kumuhoji ambapo alimweleza alikuwa ametumia dawa za kutibu ugonjwa wa UTI.
Alisema baada ya kuhojiwa kwa kina binti huyo alisema aliingia katika nyumba hiyo ya kulala wageni tangu Machi 15, 2020 akiwa na lengo la kuharibu ujauzito aliokuwa nao na alieleza alitumia dawa za aina mbalimbali bila mafanikio na kwamba ndipo Machi 18, 2020 akabadilishiwa dawa na kutimiza lengo lake.