MHAGAMA - TUNATAKA SHUGHULI ZA UCHAGUZI MKUU 2020 ZIFANYIKE JENGO JIPYA LA NEC


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, amekagua hatua ya ujenzi wa jengo la Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilizopo eneo la Njedengwa Jijini Dodoma na kusema kuwa serikali imedhamiria shughuli za Uchaguzi Mkuu mwaka huu kufanyika kwenye jengo hilo jipya la Tume hiyo.

Amebainisha hayo wakati alipofanya ukaguzi wa maendeleo ya Ujenzi wa majengo ya Tume hiyo, ljana tarehe 10 Februari, 2020, ambapo amekagua hatua za ujenzi wa ofisi za Tume hiyo kwa kukagua  Jengo Kuu la Ofisi, Jengo la kutangazia matokeo na ghala la kuhifadhi vifaa .

Kukamilika kwa majengo hayo itakuwa ni  utekelezaji wa maelekezo ya Mhe.Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa aliyoyatoa mwezi Novemba mwaka jana, ambaye aliitaka tume hiyo kuhakikisha ujenzi wa Ofisi za Tume hizo unakamilika   kwa wakati,  ili shughuli za uchaguzi Mkuu wa  mwaka huu zinafanyike kwenye majengo hayo.

Chuo kikuu- Ardhi na Kampuni ya Ujenzi ya Jeshi la Kujenga Taifa- SUMA JKT CCL ndio wanaohusika na shughuli za ukandarasi wa majengo hayo.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni idara huru iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997, ambapo kwa kipindi chote hicho tangu kuanzishwa kwake Tume hiyo haijawahi kumiliki Jengo lake lenyewe, hivyo mnano mwaka 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alikubali ombi la Tume hiyokujenga jingo lake.

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post