BASHE: VIJANA LIMENI NA KUUZA POPOTE, SERIKALI HAITOWAINGILIA


 Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewataka vijana nchini kuzalisha kwa wingi mazao ya kilimo kwa kuwa serikali haitowaingilia kupanga bei wala mahala pa kuuza.

Ametoa kauli hiyo jana mjini Chato wakati alipofungua kongamano la vijana katika kilimo kujadili fursa za kuongeza ajira na uhakika wa kipato kwa vijana wa mikoa ya Geita,Shnyanga na Kagera.

Bashe alisema Wizara ya Kilimo inatekeleza agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli la kutowazuia wakulima kuuza mazao yao mahala popote ndani na nje ya nchi na kutopanga bei elekezi.

“ Rais Magufuli alishatoa maelekezo kwa wizara yetu kutompangia au kuzuia mkulima yeyote kuuza mazao yake mahala popote anapotaka ndani na nje ya nchi” alisema Naibu Waziri.

Bashe amewaeleza vijana uwepo wa fursa kubwa ya kuzalisha mazao ya chakula na biashara kwenye mikoa ya kanda ya ziwa kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji hivyo ni muda vijana wakabadili fikra kuona kilimo ni ajira na uchumi kwao.

Bashe ameongeza kusema Taifa limekuwa salama kutokana na mchango mkubwa wa wakulima nchini kwani wameweza kuhakikisha usalama wa chakula unakuwepo na alitumia fursa hiyo kuwapongeza wakulima kwa kuendelea kuzalisha vizuri.

Naibu Waziri huyo aliwafahamisha vijana kuwa suala la kujiunga katika vikundi vya uzalishaji kupitia kilimo ni muhimu kwani linatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2015-2020 inayosisitiza kuwa ushirika ndio nguzo ya kukuza uchumi wa Taifa.

Katika hatua nyingine Bashe amezipongeza benki za NMB na CRDB kwa uamuzi wao uliofanikisha ununuzi wa zao la pamba mwaka 2019 na kuwezesha wakulima hususan kanda ziwa kupata manufaa ya jasho lao.

“ Mwaka huu nimetembelea zaidi taasisi za fedha kuliko wakulima kwa lengo la kutafuta suluhu ya changamoto za wakulima kukopesheka na upatikanaji wa masoko ya uhakika” alisema Bashe.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chato Charles Kabeho akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita aliwasihi vijana kuanza kubadilika na kulima mazao ya kudumu kama parachichi,maembe,kahawa na korosho kwani yatawasaidia kuwa na uhakika wa kipato uzeeni pale nguvu zikipungua” alisema Kabeho.

Kabeho aliwahakikishia vijana hao kuwa mkoa wa Geita una fursa nyingi na uhakika kutokana na uwepo wa ardhi nzuri yenye rutuba,uwepo wa ziwa Victoria na mahitaji makubwa ya chakula kwenye maeneo ya uchimbaji madini.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Eliud Mwaiteleke aliipongeza serikali ya awamu ya Tano kwa kuwezesha vijana wengi kupata mikopo kupitia halmashauri inayosaidia kuboresha kazi za vijana.

Mwaiteleke alisema katika mwaka 2018/2019 halmashauri ya Chato ilitoa mikopo kwa vijana,wanawake na walemavu yenye thamani ya shilingi milioni 119.

“ Katika halmshauri yetu tunakosa vijana wenye utayari kujitokeza katika vikundi kwani fedha ipo ya kutosha” alisema Mwaiteleke na kuwasisitiza vijana kubadili fikra kuona kilimo ni ajira ya uhakika.

Kongamano hilo limefunguliwa leo na linashirikisha vijana 203 toka mikoa ya Geita,Shinyanga na Kagera likiratibiwa na Wizara ya Kilimo na wadau wa sekta hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post