SERIKALI ITAENDELEA KUSIMAMIA MIRADI YA KIMAKATAKATI ILI KUWAHUDUMIA WATANZANIA


Na Eleuteri Mangi, WHUSM-Dodoma
Serikali itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia miradi mikubwa ya kitaifa ya kimkakati ili taifa liendelee kusonga mbele katika sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.  


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo lililofanyika leo jijini Dodoma. 


Miradi ambayo wizara itaendelea kuisimamia ni pamoja na kuendeleza na kutekeleza shughuli za kukuza utamaduni nchini, kuendelea na utaratibu wa kufufua Mfuko wa Sanaa utakaojumuisha Utamaduni, kufuatilia namna ya kuondokana na utata wa mapato yanayopatikana katika viwanja vya au kuboresha mapato hasa kwa kuboresha zaidi mifumo kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar es Salaam. 


“Niwahimize wajumbe wa Baraza  na Wafanyakazi  kutoa ushirikiano wa kutosha  kwa viongozi Wakuu wa Wizara ili Wizara iendelee kuwezesha  kukidhi matarajio ya Serikali katika kuwahudumia Wananchi” alisema Naibu Waziri Shonza.    


Aidha, Naibu Waziri Shonza amehimiza Wizara kuendelea kuliimarisha Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ili liweze kutekeleza kazi ya kukitangaza Kiswahili duniani kote na kuimarisha huduma za ukalimani wa lugha pamoja na kuendelea kuratibu Mradi wa Ukombozi wa Bara la Afrika. 


Katika kutekeleza wajibu wake wa kuwapa wananchi haki yao ya kupata habari, Naibu Waziri amesema Serikali inaendelea kutangaza mafanikio yanayopatikana kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati ikizingatiwa mwaka huu pia kuna kipindi muhimu cha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.   


Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbas amewataka watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia wajumbe wa Baraza hilo kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa haraka na wakati kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, na miongozo ya utumishi wa umma ili kuwa na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi. 


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango Bernard Lubogo pamoja na Happiness Kalokola kutoka Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani wamesema kuwa watafanyakazi kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali ili kukidhi matarajio ya Watanzania pamoja na wananchi kwa ujumla kupitia Idara za kisekta za Habari, Maendeleo Utamaduni, Maendeleo ya Sanaa na Maendeleo ya Michezo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527