WATAALAMU WAZUNGUKA STENDI,SOKONI KUTOA ELIMU YA VIRUSI VYA CORONA

Na Amiri Kilagalila,Njombe

Kufuatia uwepo ugonjwa wa virusi vya Corona nchini Tanzania,halmashauri ya mji Njombe imeanza kutoa elimu kwa wananchi wa halmashauri hiyo ili kuweza kuchukua hatua stahiki za kuepukana na maambukizi zaidi ambapo Idara ya afya imeanza kutoa elimu katika maeneo ya stendi,masoko,taasisi za kifedha na hoteli kuhusu dalili na njia za kujikinga na virusi hao.

Mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Njombe Dkt.Yesaya Mwasubila amewataka wananchi kuhakikisha kuwa wananawa mikono kwa kutumia maji yenye dawa kila wakati wanapokua katika maeneo ya huduma mbalimbali na amezitaka taasisi zote zinazotoa huduma kuhakikisha kuwa wanaweka maji na kutoa maelekezo kwa yeyote anayeingia au kutoka kunawa mikono ili kuepusha maambukizi.

Mwasubila amesema kwa sasa halmashauri imetenga eneo maalumu katika Kituo cha Afya Ihalula ambapo endapo kutabainika mgonjwa mwenye dalili za virusi vya Corona atawekwa chini ya uangalizi wa siku 14 katika kituo hicho.

Kinga ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya COVID 19 vinavyosababisha homa ya CORONA ni pamoja na kuepuka msongamano, kunawa mikono vizuri kwa maji safi yanayotiririka na sabuni, au maji yenye dawa, kutumia vitakasa mikono, kutumia vikinga pua na mdomo (masks) kwa wale wanaopiga chafya au kukohoa, kuepuka kugusana na kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post