CCM MBOGWE YAITAKA SERIKALI KUDHIBITI WANAUME WANAOWAPA MIMBA WANAFUNZI

Na Salvatory Ntandu - Geita
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbogwe mkoani Geita kimeishauri serikali kuchukua hatua za haraka kuwadhibiti wanaume wanaowapa mimba wanafunzi kutokana na kukithiri kwa matukio mimba katika shule za msingi na sekondari.

Ushauri huo umetolewa Machi 5 mwaka huu na Katibu wa (CCM) wilaya ya Mbogwe, Grace Shindika, kwenye kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho, baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo Martha Mkupas.

Alisema serikali inapaswa kuhakikisha inawakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaume wanaowapa mimba wanafunzi kwani vitendo hivyo vimekuwa vikikatisha ndoto zao za kuendelea na masomo.

“Wakamateni wanaojihusisha na mapenzi na wanafunzi ili kutokomeza vitendo hivi,serikali ya awamu ya tano chini Rais Dk. John Pombe Magufuli imetoa fursa ya elimu bure kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne,haiwezekani tukavifumbia macho vitendo hivyo”,alisema Shindika.

Alifafanua kuwa kwa kipindi cha Julai hadi Disemba mwaka 2019 wanafunzi wanne kutoka katika shule za sekondari walipata mimba katika wilaya hiyo na kusababisha kushindwa kuendelea na masomo lakini bado suala hilo halijapewa kipaumbele ili kulidhibiti.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 kwa kipindi cha Julai hadi Disemba,Mkuu wa wilaya ya Mbogwe Matha Mkupas alisema kwa kipindi hicho matukio ya wanafunzi kupata mimba yalikuwa manne katika shule za sekondari ambapo mashauri matatu tayari yameshafunguliwa.

Alifafanua kuwa kwa kipindi hicho shule zilizoripotiwa wanafunzi wake kupata mimba ni pamoja na ya sekondari Masumbwe (1) Iponya (1) Kanegere (1) na Ikunguigazi (1) ambapo tayari jeshi la polisi wilayani humo linaendelea na mashauria matatu katika mahakama za wilaya.

“Ili kutokomeza mimba katika shule zetu ni lazima tuwaelimishe wazazi kuacha vitendo vya kuharibu ushahidi kwa kufanya makukubaliano pindi kunapotokea kwa tukio la mimba kwa wanafunzi na kusababisha watuhumiwa kutoroka au kuwatorosha wanafunzi wenye mimba”,alisema Mkupas.

Kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho, kimepokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015 kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2019.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post