TAASISI ZA KIFEDHA NCHINI ZATAKIWA KUACHA URASIMU KATIKA MIKOPO

Na Salvatory Ntandu - Kahama

Serikali imezitaka Taasisi za kifedha nchini kuacha urasimu katika utoaji wa mikopo kwa wawekezaji wa viwanda wa ndani ili kuwasaidia kukuza mitaji yao hali ambayo itachangia kuongeza ajira.

Kauli hiyo imetolewa Machi mosi na Makamu wa Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Ali Idd wilayani, Kahama mkoani Shinyanga katika ziara yake ya kwanza baada ya kutembelea na kukagua eneo la ujenzi wa viwanda vitatu katika eneo la Chapulwa vinavyojengwa na KOM GROUP OF COMPANIES.

Alisema kuwa baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zitoa masharti magumu kwa wawekezaji wa ndani pindi wanapohitaji kukopeshwa fedha kwaajili ya kukuza biashara zao na kusababisha wengi wao kushindwa kuwekeza kwa tija.

“Nizitake taasisi hizi zitambue umuhimu wa wawekezaji wetu wa ndani kama vile kampuni hii ya KOM ambayo inaendelea na uwekezaji katika eneo hilo la Chapulwa,riba zikipungua nina imani watanzania wengi watanufaika kwa kupata mikopo ambayo itasaidia kukuza uwekezaji wao”,alisema Balozi Idd.

Alifafanua kuwa Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli imejikita katika uanzishwaji wa viwanda hivyo ni budi kwa taasisi hizo kuunga mkono juhudi za kuelekea katika uchumi wa kati na kuwawezesha wananchi wengi kupata ajira za kudumu sambamba na kuongeza uchumi wa taifa.

“Mkoa wa shinyanga mmetia fora katika uhamasishaji wawekeza wa ndani katika ujenzi wa viwanda nimekagua eneo hili ambako kunajengwa viwanda zaidi ya vitatu ambapo watanzania zaidi ya 2000 watapata ajira”,alisema Balozi Idd.

Naye mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alitoa rai kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika mkoa wa Shinyanga kutokana na wingi wa fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa huo.

“Katika eneo hili la Chapulwa mkoa wa Shinyanga tumetoa viwanja bure kwa wawekezaji huyu wa kampuni ya KOM kama kuwapa motisha ya kuwahamasisha kuwekeza katika mkoa wetu sambamba na kuandaa mazingira rafiki kwao”,alisema Telack.

Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya KOM GROUP OF COMPANIES,Braison Edward alisema kuwa gharama za uwekezaji wa kiwanda hicho ni zaidi ya dola milioni 10 za Kimarekani na viwanda vitakavyojengwa ni vya maji,soda na kusaga nafaka.

Balozi Seif Alli Idd yupo mkoani Shinyanga katika ziara ya siku tano akiwa ni mlezi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga ,akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM.
Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na kwa kutowapa mikono viongozi kutekeleza agizo la Waziri wa Afya Ummy mwalimu kuhusu Virusi vya Corona.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga  Mabala Mlolwa akiwa amekiti na mgeni wake Balozi Seif Ali Idd katika sofa katika eneo la Bukondamoyo
Mkuu wa mkoa wa shinyanga zainabu telack akiwa ameketi kwenye sofa na Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika eneo la viwanda vidogo la bukondamoyo katika eneo la halmashauri ya mji wa kahama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post