JAFO AINGILIA KATI SAKATA WANAFUNZI WALIOKOSA USAFIRI BAADA YA SHULE KUFUNGWA KISA CORONA

Mwandishi wetu OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo ameagiza Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi na Wakuu wa shule nchini,kuhakikisha wanafunzi waliokosa usafiri wanasafirishwa badala ya kuwaacha wakizagaa kwenye vituo vya mabasi.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dodoma kutokana na baadhi ya maeneo wanafunzi wakionekana kupata adha ya usafiri licha ya serikali kutoa maelekezo ya namna ya kuwasafirisha wanafunzi hao hadi makwao.

Amesema serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ilitoa maelekezo ya kufunga shule zote na vyuo vikuu kwa kipindi cha siku 30  kutokana na ugonjwa wa Corona na Katibu Mkuu alishaandika barua kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa kwamba uwekwe utaratibu mzuri kwa vijana hao kuanzia Machi 17-20 wa kuwasafirisha hadi makwao kwa usalama na amani.

Waziri. Jafo  amesema  agizo hilo lilitolewa kwa viongozi hao kusimamia  vizuri zoezi hilo lakini baadhi ya maeneo utaratibu haukwenda vizuri hadi leo wanafunzi wa bweni wameruhusiwa kwenda vituoni kutafuta magari wenyewe na hivyo kusababisha wanafunzi kutangatanga sana.

“Tumesikia kwenye maeneo ya Moshi na Morogoro tumeona wanafunzi wa Dakawa wakitangatanga kituo cha mabasi Msamvu na Maeneo mengine, katika hili halikubaliki hata kidogo,”amesema Mhe. Jafo

Ametoa pongezi kwa Mkuu wa Shule ya Kilakala iliyopo Morogoro na Mkuu wa Shule ya Dodoma Sekondari kwa kuweka utaratibu mzuri wa kusafirisha wanafunzi hao.

“Kilakala alihakikisha wanafunzi wake wote anawakodia mabasi yanawachukua shuleni na hadi leo(jana) alikuwa amebaki na wanafunzi 30 wanaoenda Mkoa wa Manyara, Kiteto na Simanyiro ambao anawasafirisha, pia Dodoma yeye hata wanafunzi wasiokuwa na nauli alikodi magari kuwasafirisha bila nauli na kuwataka wazazi watume kwake nauli hizo ili alipe gharama za usafiri,”amesisitiza Mhe. Jafo

Aidha ameagiza viongozi hao wahakikishe wanafunzi ambao hawajapata usafiri hadi sasa waratibu na kuwasafirisha kwenda majumbani kwao kwa salama na amani na hatarajii kuona wakitangatanga kwenye maeneo yao.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post