UDSM YATOA SAA 48 WANAFUNZI WOTE WAONDOKE CHUONI

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) nchini Tanzania kimewataka wanafunzi wote kuhakikisha ifikapo Ijumaa Machi 20, 2020 wawe wameondoka kurejea nyumbani.

UDSM imetoa taarifa hiyo leo Jumatano Machi 18,2020 ikiwa ni saa chache kupita tangu Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa atangaze kuvifunga vyuo vyote kutokana na kujikinga na virusi vya ugonjwa wa corona (CODIV-19).

Agizo hilo la Majaliwa amelitoa baada ya wagonjwa wawili zaidi raia wa kigeni kubainika kuwa na virusi vya corona wakiwa Dar es Salaam na Zanzibar hivyo kufikisha idadi ya waliobainika nchini humo kuwa watatu.

Katika taarifa ya Makamu mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye imesema katika kutekeleza maelekezo na ushauri wa Serikali kwa lengo la kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo, shughuli zote za masomo chuoni hapo zimesitishwa kuanzia leo Machi 20 2020 hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo.

“Kutokana na masomo kusitishwa, wanafunzi wote, wa programu zote, walioko likizoni wanatakiwa kubaki nyumbani huko waliko, hadi hapo watakapotaarifiwa kurejea chuoni,” amesema Profesa Anangisye

Makamu mkuu huyo wa chuo amesema, “wanafunzi wote wa programu zote, ambao kwa sababu mbalimbali bado wapo katika kampasi yoyote ya chuo wanatakiwa kuwa wameondoka chuoni ifikapo Ijumaa Machi 20, 2020, kwenda nyumbani hadi hapo watakapotaarifiwa kuwa chuo kimefunguliwa tena.”

Amesema shughuli nyingine zote za Chuo zitaendelea kama kawaida kwa kuzingatia maelekezo kuhusu udhibiti wa kuenea kwa ugonjwa wa corona.
CHANZO- MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post