BLOGA MBARONI KWA KUCHAPISHA MTANDAONI TAARIFA ZENYE KUZUA HOFU KUHUSU CORONA

Mwendeshaji wa Mitandao ya Kijamii Bloga (Blogger) Robert Alai anashikiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga nchini Kenya kufuatia madai ya kuchapisha ujumbe wa kuzua hofu miongoni mwa watu mitandaoni kuhusu Virusi vya Corona (Covid-19).

 Bloga huyo aliagizwa kufika katika Idara ya Upelelezi mnamo Ijumaa, Machi 20,2020 kuandikisha taarifa kufuatia ujumbe wa kuzua hofu aliouchapisha mitandaoni kuhusu janga la coronavirus  kabla ya kukamatwa na kusafirishwa hadi kituo cha polisi cha Muthaiga.

 Bloga Robert Alai atalazimika kulala kizuizini wikendi nzima kwa madai alichapisha ujumbe wa kuzua hofu mitandaoni kuhusu janga la coronavirus. 

 Inadaiwa kwamba, Alai alichapisha ujumbe kwenye ukurasa wa Twitter kwamba watu kadhaa wameaga dunia Mombasa baada ya kuambukizwa virusi vya corona. 

Mshukiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu kujibu mashtaka hayo.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kwenye kikao na waandishi wa habari mnamo Alhamisi alionya kwamba serikali itamchukulia hatua kali yeyote ambaye atasambaza ujumbe wa kupotosha kuhusu maradhi hayo. 

"Ningependa kuwaomba wananchi kujiepusha na kusambaza jumbe zozote za kupotosha. Uvumi umekuwa ukisambazwa mitandaoni kwamba Nairobi itafungwa na kwamba tutawatuma watu mashambani.....haya ni mambo yasiyo ya ukweli. Uvumi huo unapaswa kukomeshwa haraka," Kagwe alisema. 

 Hii sio mara ya kwanza kwa bloga huyo kujipata pabaya kwani mwaka jana Juni, alikamatwa kwa madai ya kusambaza picha za polisi waliouawa katika shambulizi la kigaidi Wajir.

 Alishtakiwa kwa usaliti na kutoa habari za kijasusi na baada ya kuzuiliwa kwa wiki mbili aliachiliwa kwa dhamana ya KSh 300,000 baada ya kukana mashtaka.

Chanzo- TUKO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527