ASKARI WA ZIMAMOTO WATAKIWA KUWA NA UPENDO KWA WANANCHI WANAOWAHUDUMIA

Na Bahati Mollel, TAA

Askari wa Zimamoto wa Kiwanja cha Ndege cha Mafia na cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) wametakiwa kuwa na upendo kwa wananchi wanaowahudumia wakati wa kufanya shughuli za kuzima moto na uokoaji katika majanga mbalimbali yanayoweza kutokea kwenye viwanja vya ndege.

Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Kamishna wa Zimamoto na Uokoaji, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Jeshi hilo Kampasi ya Dar es Salaam na Chogo kilichopo Handeni Tanga, DCF Kennedy Komba wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya kujengeana uwezo kwa Wazimamoto hao yaliyokuwa yakifanyika kwenye Jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3).

DCF Komba amesema anatarajia wahitimu hao wapatao 54 watatoa huduma bora katika vituo vyao vya kazi kutokana na kujengewa uwezo mkubwa, ambapo anatarajia siku moja jeshi hilo kupitia vituo vya viwanja vya ndege Tanzania, watatunukiwa cheti au tuzo ya heshima kutokana na kufanya kazi iliyotukuka.

“Kazi yenu ni ya wito mnatakiwa kuwa na upendo na watu mnaokwenda kuwahudumia wakati wa majanga, msitumie lugha mbaya na ni aibu kwa askari wakati wa maokozi wewe unaanza kumpekua mhanga na kuanza kumuibia labda simu au fedha alizokuwa nazo mifukoni, mnachotakiwa ni kuonesha upendo wa hali ya juu kuanzia mwanzo hadi mwisho wa zoezi la uokoaji,” amesema DCF Komba.

Pia aliwataka wahitimu hao kutunza afya zao kutokana na kazi yao inahitaji wawe askari hodari na shupavu, kwani akiwa mgonjwa hataweza kazi ya uokoaji wakati wa
majanga kwani inahitaji nguvu na akili nyingi.

“Hapa naona wahitimu wote ni vijana nawaambia wazi ukimwi unaua na ukimwi unadhoofisha mwili, hivyo mjitunze kwani ukiwa na afya mgogoro hautaweza kuhimili mikikimikiki ya kazi yetu, na wakuu wenzangu mnapokuwa na nafasi ya kukutana na askari msichoke kuwaeleza juu ya kutunza afya zao,” amesisitiza DCF Komba.

Halikadhalika amewataka wahitimu kuwa mabalozi wazuri maeneo wanayoishi kwa kuwa na vifaa vya zimamoto majumbani mwao ukiwemo mchanga mkavu unaowekwa kwenye ndoo na ‘Fire extinguisher’ pia kutoa maelekezo mbalimbali kwa wanaowazunguka endapo kutatokea janga la moto au uokoaji wa majanga mengine, ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na moto.

DCF Komba ameishukuru Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwa kufanikisha mafunzo hayo, na ameiomba isichoke kuwajengea uwezo askari hao ili
waweze kufanya kazi bora zaidi kwa manufaa ya taifa nzima la Tanzania.

Katika hatua nyingine DCF, amemshukuru Kamishna Msaidizi (Mstaafu), Christom Manyologa kwa kuwanoa askari hao na kumuomba kuendelea kufanya hivyo pindi
atakapohitajika wakati mwingine, pamoja na wastaafu wengine.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Zimamoto na Uokoaji kwa upande wa Viwanja vya Ndege Tanzania, ACP Bakari Mrisho alisisitiza askari kuwa na upendo na kuthamini kazi yao kwa kuwa viwanja vya ndege vinawategemea.

“Tuwe tayari kwa matukio na tuangalie mafunzo yanayolenga kazi yetu na sio kulazimisha mafunzo ambayo hayaendani na kazi yetu hii,” amesema ACP Mrisho.

Naye Mkufunzi ACP Manyologa amewataka washiriki kujiandaa wakati wote tayari kwa matukio, ambao alitoa mfano mwaka juzi katika kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ilitua ndege kubwa ya A380 ya shirika la Emirates kwa dharura ambayo ina abiria zaidi ya 500 na inakiasi kikubwa cha mafuta na waliweza kuwa tayari kwa lolote ambalo lingeweza kutokea na ndege ilitua na kuondoka salama.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post