WIZARA YA AFYA YAKABIDHIWA RASMI HOSPITALI YA RUFAA MAWENI

Na. Catherine Sungura– Kigoma

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekabidhiwa rasmi hospitali ya rufaa ya mkoa maweni iliyopo mkoani Kigoma.

Akikabidhiwa hospitali hiyo Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa anashukuru sekretarieti ya mkoa kwa kuisimamia hospitali hiyo pamoja na watumishi katika kipindi hicho na hivyo kuwezesha wananchi kupata huduma zinazostahili.

“Pamoja na makadhibiano tutaendelea kushirikiana kwa ukaribu na ofisi yako RAS na bado utaendelea kuwasimamia watumishi hawa kwani wapo mkoani kwako”.

Aidha, Dkt. Chaula amesema wizara yake wametengeneza mkataba kati ya Wizara na RAS katika eneo la usimamizi hasa ya majengo ili yaweze kubaki kwenye uimara unaohitajika.

“Tunawashukuru watendaji wa ofisi ya katibu tawala kwa kazi nzuri waliyoifanya ya usimamizi wa hospitali hiyo hadi sasa tunakabidhiana, tutakwenda kuzisoma nyaraka hizi moja baada ya nyingine, maana ni mali za Serikali, mmetueleza kuna madeni tutayapitia na kuyafanyia kazi,” alisema.

Naye Katibu Tawala wa mkoa wa kigoma Rashid Machatta alisema kwamba bado ataendelea kushirikiana kwa ukaribu na watumishi wa hospitali hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao ili wananchi waweze kupata huduma bora

“ Watumishi sisi bado ni wamoja, tutashirikiana bega kwa bega ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma zilizo bora”.Alisema Rashid Machatta.

Wakati huo huo Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Osmond Dyegula alisema hospitali hiyo ina jumla ya watumishi 233, kwa wastani wanaona wagonjwa kati ya 300 hadi 330 kwa siku kutokana na takwimu za mtuha za mwaka 2018/19.

Wizara ya afya imekabidhiwa hospitali hiyo ikiwa ni agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kuhamishia usimamizi huo wizara ya afya mwaka 2017 kutoka chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post